Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tatizo la Kukatika Umeme katika Mitambo ya TBC kushughulikiwa haraka
Aug 12, 2020
Na Msemaji Mkuu

Fundi Mitambo wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Bw. Hamis Kalanje akimuonyesha mitambo ya kurushia matangazo ya redio iliyopo Kihipe mkoani Lindi Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe (kushoto),wakati alipotembelea kituo hicho mnamo Agosti 11,2020

Na Shamimu Nyaki –WHUSM, Lindi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwamba suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Mikoa ya Lindi na Mtwara linalosababisha mitambo ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kushindwa kufanya kazi ipasavyo linapaswa kushugulikiwa kwa haraka.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo Agosti 11, 2020 alipokua katika ziara ya kukagua mitambo ya TBC iliyopo Kipihe mkoani Lindi ambapo amesema suala hilo ni la kisera hivyo ataliwasilisha Wizara ya Nishati ili litafutiwe ufumbuzi wa kudumu.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Lindi wakati wa ziara yake mkoani hapo ya kukagua usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na kuzungumza na wadau wa sekta anazozisimamia mnamo Agosti 11,2020.Kulia ni Katibu Tawala  wa Mkoa  huo Bibi.Rehema Madenge.

“Maeneo ya kimkakati hayapaswi kukosa umeme wa uhakika, eneo hili la Kipihe ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati ambayo yanasaidia shirika letu la utangazaji TBC kutoa habari kwa wananchi wa mikoa ya kusini hivyo umeme lazima uwe wa uhakika utakaowezesha mitambo hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na muda wote”,alisema Mhe.Mwakyembe.

Mhe. Mwakyembe ameongeza kuwa TBC ni chombo cha umma ambacho kina wajibu wa kuelezea wananchi nini Serikali imefanya katika nchi na inatarajia kufanya nini katika siku zijazo hivyo changamoto yoyote inayojitokeza katika chombo hicho ni lazima itafutiwe ufumbuzi wa haraka.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na  uongozi wa Mkoa wa Lindi na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wakati wa ziara yake mkoani hapo ya kukagua usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na kuzungumza na wadau wa sekta anazozisimamia mnamo Agosti 11,2020.

Kwa upande wake Mhandisi wa Shirika hilo Bibi Upendo Mbele amesema kwamba usikivu wa shirika hilo umeendelea kuimarika ambapo maeneo mengi yanafikiwa kwa ubora unaotakiwa kufuatiwa kufungwa mitambo ya kisasa katika mkoa huo.

Bibi Upendo ameongeza kuwa ndani ya wiki mbili zijazo eneo la Kipihe litawekewa jenereta ambalo litasaidia mitambo isizimike pale umeme unapokatika hali ambayo inasababisha matangazo ya redio kukatika, huku akieleza kuwa Mwaka wa fedha 2020/2021 TBC imetenga fedha kwa ajili ya kuimarisha studio ya Kanda ya Kati Dodoma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi