Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TASAC Watoa Elimu ya Usalama kwa Wavuvi Wilayani Mkinga
Apr 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Oscar Assenga - Mkinga

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Tanga limekutana na wavuvi, wamiliki wa vyombo wa Vijiji vya Petukiza na Moa wilayani Mkinga kwa ajili ya kutoa elimu ya usalama wa vyombo vya majini na umuhimu wa kuwa na vifaa vya kujiokolea ikiwemo maboya wakati wanapokuwa wakifanya shughuli zao za majini kila siku.

Akizungumza wakati akitoa elimu hiyo, Ofisa Mfawidhi wa Shirika hilo mkoani Tanga, Captain Christopher Shalua alisema vyombo vidogo vya majini vinapaswa kuzingatia usalama na utunzaji wa mazingira ikiwemo matumizi sahihi ya maboya ya kujiokolea.

Alisema pia ni muhimu wakatambua matumizi sahihi wakati wa kuyavaa kutokana na muhimu kuyavaa muda wote wanapokuwa kwenye shughuli za uvuvi au kusafiri majini ili kuweza kuwasaidia pindi wanapokumbana na majanga mbalimbali.

Captain Shalua alisema walikuwa wakiwaelimisha wavuvi ili waweze kupata uelewa juu ya matumizi sahihi ya vifaa ambavyo kwa mujibu wa sheria vinapaswa kuwepo kwenye vyombo.

“Lakini pia vifaa vingine ambavyo vinapaswa kuwepo kwenye vyombo vyenu ni vya kuzimia moto na vile kwa ajili ya huduma ya kwanza kwani vina umuhimu wakati wa dharura ni wakati gani mvuvi anaweza kuvitumia ili viwe msaada kwake”Alisema Captain Shalua.

Hata hivyo alisema kwa mfano vyombo vingi vya uvuvi vinatumia mafuta ya petrol kwa ajili ya kuendesha mashine zao kwa hiyo moto unapowaka kutokana na mafuta hayo hawawezi kuzima kwa kutumia maji badala yake wanaweza kuuzima kwa kutumia mchanga au poda maalumu iliyopo kwenye mitungi.

Aliongeza kwamba wanaweza pia kutumia mapovu maalumu yaliyopo kwenye mitungi hivyo elimu yao ilijikita kwenye maeneo hayo ili iweze kuwasaidia wavuvi wanapokuwa mbali na nchi kavu wanapopata majanga waweze kujisaidia na kuokoa mali na kuwaepusha na kupoteza maisha.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kijiji cha Petukiza Kata ya Moa wilayani Mkinga, Mrashi Kea Kasim alisema wavuvi wamesikiliza elimu hiyo na changamoto kubwa wavuvi wamekuwa wakifa baharini kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kujiokolea.

“Tunaiomba Serikali ione namna ya kutusaidia wavuvi nasi baadae tuweze kununua kwani ni ukweli kwamba wavuvi wanapotoka nchi kavu kwenda baharini kuna urefu mkubwa na mtu anaachwa mita 20 pekee yake bila msaada na wakati mwingine anapopata dhoruba kujiokoa inakuwa ngumu”, Alisema.

Alisema kutokana na kwamba Serikali inaingiza mapato makubwa sana kutokana na ukusanyaji wa maduhuli hivyo wanaiomba iwaangalie kwa kwa kuwawezesha ili baadae waweze kujinunulia wenyewe vifaa vya usalama.

Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji cha Petukiza, Kasim Ally alisema kwamba elimu hiyo itakwenda kuwasaidia wakati wakitekeleza shughuli zao mbalimbali za uvuvi.

“Kwanza nilishukuru Shirika la TASAC kwa kuona umuhimu wa kuja kutupa sisi wavuvi elimu na tunahaidi tutakwenda kuifanyia kazi", Alisema Kasim.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi