Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzanite Kuwa na Hati ya Utambulisho Kimataifa
Aug 25, 2018
Na Msemaji Mkuu

 

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Serikali imesema inafanya utaratibu wa kuwa na Hati ya Utambulisho wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite, ambayo yanapatikana katika nchi ya Tanzania pekee katika vilima vya Mirerani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 25 Agosti na Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa Semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo imefanyika Makao Makuu ya Wizara, jijini Dodoma.

Waziri Kairuki amesema kuwa, serikali inataka kuona kuwa dunia inafahamu kuwa, madini hayo yanapatikana Tanzania pekee na kuhakikisha kwamba yanajulikana zaidi.

Semina ya wabunge imefanyika kufuatia maelekezo ya Kamati hiyo ambayo ilitaka kufahamu kuhusu mwenendo mzima wa Madini ya tanzanite, biashara na udhibiti wa madini hayo baada ya kujengwa kwa Ukuta wa Mirerani unaozunguka migodi ya madini ya tanzanite, Muundo wa Wizara ya Madini, Tume ya Madini na majukumu yao.

Waziri Kairuki amesema kuwa, Wizara imepata fursa ya kuwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo mikakati ya serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini hayo na mipango madhubuti ambayo serikali inakusudia kuifanya ili kuhakikisha kwamba rasilimali madini inalinufaisha taifa na hatimaye sekta ya madini iweze kufikia asilimia 10 ya machango wake katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.

Ameongeza ni  kikao ambacho kimekuwa na manufaa kwa upande wa Serikali kwa kuwa imetoa elimu kwa Kamati hiyo kuhusu yale ambayo serikali imefanya na inayokusudia kufanya kuhusuiana na madini  ya tanzanite lakini pia serikali imepata wasaa wa kupokea maoni, mapendekezo na maelekezo kutoka kwa wabunge ambayo yatawezesha kupeleka mbele sekta ya Madini.

Mbali ya tanzanite, Waziri Kairuki amewaeleza wabunge hao kuhusu mkakati wa serikali kuanzisha Mineral Exchange ambapo amesema tayari wizara imeshaandaa timu ya wataalam ili kwenda kujifunza na kufanya utafiti katika nchi nyingine ili suala hilo liweze kufanyika kwa ubora .

Pia, ameeleza kuwa, Wabunge wa Kamati hiyo, wamepata fursa ya kufahamu majukumu ya Wizara baada ya kuundwa kwa Tume ya Madini, majukumu ya tume ya madini na mahusiano ya kiutendaji kati ya Tume na Wizara.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile, amesema kuwa, kamati imebaini kuwa, Serikali imechukua hatua nyingi za kulinda na kudhibiti madini ya tanzanite ikiwemo  kudhibiti utoroshaji wa madini hayo. “Kama kamati tumeona mnyororo mzima wa thamani ya madini ya tanzanite, awali tulikuwa hatunufaiki kama taifa,” amesema Ditopile.

Awali, akiwasilisha mada kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini ya tanzanite na usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ndani ya ukuta, Afisa Madini Mkazi wa Mirerani Mhandisi David Ntalimwa, amezungumzia sababu za kushuka kwa mapato na kueleza kuwa, kunategemea kiwango cha ubora na sifa za madini husika.

Ameongeza kuwa, kutokana na mazingira hayo, kiwango cha thamani ya madini na tozo ya mrabaha kitakuwa tofauti kutegemea na mwezi na uzalishaji uliopo.

Akizungumzia sababu za utoroshaji wa madini ya tanzanite, Mhandisi Ntalimwa amesema kuwa, zinatokana na uwezo mdogo wa kusanifu na kuongeza thamani na kunga’risha madini ya vito na hivyo watu kutamani kuuza tanzanite ghafi.

Pia, amesema utoroshaji wa madini unatokana na kukwepa kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa na serikali ili kujipatia faida kubwa, kuwepo kwa raia wa kigeni nchini wanaofanya biashara ya madini kinyume na sheria kwa kushirikiana na wazawa na kukosekana kwa masoko ya uhakika ya kuuzia madini yanayozalishwa.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini baada ya kujengwa ukuta amesema kuwa, serikali imeimarisha ulinzi na ukaguzi getini kwa kutumia vikosi vya ulinzi na usalama, kuzuia magari kuingia na kutoka ndani ya ukuta, watu kuingia ndani ya ukuta kwa vitambulisho maalum.

“ Sasa watu wanaingia kwa utaratibu maalum tofauti na walivyozoea awali. Ukuta umeleta utaratibu mzuri na si kero, kama baadhi ya watu wanavyodhani,” amesisitiza Ntalimwa.

Amezitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuzuia Mabroker kwenda migodini na badala yake kutakiwa kusubiria madini getini, uthaminishaji madini kufanyika ndani ya ukuta na serikali kujenga jengo lenye ofisi ya ukaguzi, uthaminishaji na ukumbi wa mabroker ndani ya ukuta.

Aidha, pamoja na kushiriki semina hiyo, pia wabunge hao wamepata fursa ya kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Jiolojia na Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, (GST).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi