Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yapongezwa Uhifadhi Ngorongoro
Oct 25, 2023
Tanzania Yapongezwa Uhifadhi Ngorongoro
Picha ya pamoja ya Majaji Wakuu kutoka Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika pamoja na baadhi ya wageni waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Majaji hao wakiwa katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro leo jijini Arusha.
Na Ngorongoro Crater, Arusha.

Majaji Wakuu kutoka Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika wameipongeza Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kuhifadhi eneo la Ngorongoro na hivyo kulifanya kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika.

Waheshimiwa Majaji wametoa pongezi hizo leo Oktoba 25, 2023 walipotembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo katika eneo hilo, na kuvutiwa  jinsi Serikali ilivyoboresha mazingira na kuimarisha uhifadhi.

Wakiongozwa na Mwenyeji wao Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Majaji Wakuu hao waliweza kutembelea vivutio mbalimbali  na kujionea uzuri wa Bonde la Ngorongoro na wanyama mbalimbali kama Faru, Simba, Tembo, Viboko, Nyati, Pundamilia, Ziwa Magadi na misitu inayopendezesha uwepo wa hifadhi hiyo.

Jaji Mkuu wa Namibia, Mhe. Peter Shivute alisema ziara yao katika eneo hilo imekuwa na tija kubwa na wamejionea jinsi Serikali inavyosimamia uwepo wa hifadhi hiyo na kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mataifa tofauti duniani.

“Tumefurahishwa na hifadhi ya Ngorongoro, kwa kweli Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhifadhi vivutio hivi, tangu tuingie Arusha tulikuwa na shauku kubwa ya kuja kujionea hali ya mambo ilivyo  kwa kweli vinaifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya utalii”, alisema Jaji Mkuu Mhe. Shivute kutoka Namibia.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zimbabwe, Mhe. Luka Malaba alisema kufika kwake katika hifadhi hiyo amejionea jinsi sekta ya uhifadhi inavyopiga hatua na kuvutia watalii wengi kuingia nchini kujionea vivutio hivyo.

Akizungumza  kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Urithi wa Utamaduni na Jiolojia, Mhandisi Joshua Mwankunda amesema hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kusimamia ustawi wa vivutio vyote vilivyopo katika eneo hilo ili kuiwezesha Serikali kupata mapato na kuboresha huduma za utalii na miundombinu wezeshi kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Mhandisi Mwankunda alisema uwepo wa hifadhi hiyo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi  bora na  shirikishi kitu kinachosaidia watalii kutoka nchi mbalimbali duniani kufika na kujionea vivutio vilivyopo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama nchini, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema Majaji Wakuu hao walikuwa na shauku kubwa ya kufika eneo la Ngorongoro hasa kutokana na sifa iliyojijengea hifadhi hiyo katika nchi mbalimbali duniani.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi