Na Shamimu Nyaki - WUSM, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu leo Mei 09, 2022 jijini Dodoma ameongoza kikao cha awali kati ya Wizara na Wawakilishi wa Waandaaji wa Tuzo za MTV Afrika kutoka nchini Afrika Kusini kujadili kuhusu Tanzania kuandaa Tuzo za Muziki za MTV (The MTV Africa Music Awards) kwa mwaka 2022/23.
Katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Yakubu ameeleza utayari wa wizara kushirikiana na Kampuni hiyo kwa kuwa ni fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka juhudi katika kuitangaza nchi ili kuvutia wawekezaji na watalii wengi duniani kuja nchini.
"Kikao cha leo kimetupa fursa ya kuona namna gani Nchi yetu itafaidika na ujio wa Tuzo hizo, tumeona Wasanii wetu watapata nafasi ya kujitangaza na kutangaza Sanaa ya Tanzania Duniani, Kuna fursa pia ya kutangaza Nchi yetu katika Utalii hivyo tumepokea wazo na tutalijadili na kutoa mrejesho wenye tija", amesema Naibu Katibu Mkuu Yakubu.
Ameongeza kuwa wizara yake itafanya Mawasiliano na Wizara nyingine ikiwemo Maliasili na Utalii pamoja na wadau wengine ili kuona namna ya kufanikisha tukio hilo kubwa la Muziki Barani Afrika ambalo likifanyika litakaribisha takriban wageni elfu 10 nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka MTV, Ndugu Kabelo Ngakane alisema kuwa wanavutiwa na Tanzania kwa kuwa imefunguka katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara ya Muziki na Utalii, hivyo ni fursa ambayo MTV itaitumia kuitangaza zaidi ulimwenguni.
Ameongeza kuwa, kufanyika kwa Tuzo hizo kutatoa nafasi kwa Wasanii mbalimbali ikiwemo wanamuziki, wachezaji (Dancers) waandaaji wa Muziki, watangazaji kupata elimu pamoja na ujuzi mbalimbali katika kukuza Sanaa zao.
Tuzo za Muziki za MTV Africa zilianza tangu Mwaka 2008 ambapo Nchi kama South Afrika Nigeria, Ghana, Uganda na nyingine zimeshaandaa Tuzo hizo.