Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali itaendelea na jitihada zake za kupunguza vifo vya wanawake wakati wa kujifungua hadi kufikia lengo la kimataifa ambalo ni wanawake 70 kati ya wanawake wote wanaojifungua ndani ya mwaka mmoja.
Rais Samia ameeleza malengo hayo ya nchi leo Machi 08, 2025, wakati akizungumza jijini Arusha katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo kitaifa yamefanyika mkoani humo.
Amesema kuwa Tanzania inaendelea na jitihada za kuboresha sekta ya afya ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa zikiwemo za ujenzi wa miundombinu, uwekaji wa vifaa pamoja na ukuzaji ujuzi na utaalam ambao umeiwezesha nchi kufanya matibabu mengi ndani ya nchi.
"Lengo la wanawake wanaofariki wakati wa kujifungua kimataifa ni wanawake 70 kwa mwaka mzima, Tanzania bado hatujafika hapo ila nina hakika ifikapo mwaka 2030, Tanzania itafikia malengo ya kimataifa", amesema Rais Samia.
Amefafanua kuwa, Tanzania imeweza kupunguza vifo vya wanawake wakati wa kujifungua ambapo wakati mkutano wa wanawake Beijing unafanyika, vifo vya wanawake wa Tanzania wakati wa kujifungua vilikuwa 1,500 kwa vizazi hai 100,000 na kwa sasa vifo hivyo ni 104 kwa vizazi hai 100,000.
Aidha, vifo vya watoto navyo vinapungua na jitihada za kupunguza zaidi vifo hivyo inaendelea.
Akizungumza kwa ujumla, Rais Samia amesema kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kisheria katika kupambana na mila kandamizi na ubaguzi kwa wanawake na watoto wa kike.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yanafanyika nchini kila mwaka huku maadhimisho hayo yakifanyika kila baada ya miaka mitano.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji."