Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameushukuru Mfuko wa nchi zinazozozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC FUND) kwa kuwekeza hapa nchini zaidi ya Dola za Marekani milioni 218 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 504, kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Nchemba, alitoa shukrani hizo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Dkt. Alkhalifa Abdulhamid Saleh ambapo walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo.
Alisema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali, ukiwemo mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, mradi wa barabara ya Kazilambwa-Chagu, barabara ya Uvinza-Ilunde – Malagarasi pamoja na kufadhili mradi wa kupambana na Umasikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF
“OPEC FUND, mmekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu katika kukuza uchumi wa nchi, kupunguza umasikini wa wananchi na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii watu wetu”, alisema Dkt. Nchemba
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua umuhimu wa Sekta Binafsi katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi na imejitahidi kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara katika sekta hiyo.
Alisema kuwa Serikali imeongeza kiwango cha mikopo kwa Sekta Binafsi kutoka asilimia 5.1 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 5.9 mwaka 2021 na kuahidi kuwa kiwango hicho kitaendelea kuongezeka kadri hali ya uchumi itakavyoimarika, pamoja na kuendelea kuimarisha sera za kiuchumi na kifedha zitakazoendelea kujenga imani kwa wawekezaji na sekta binafsi.
Aidha, Dkt. Nchemba alitumia fursa ya mkutano huo kuliomba Shirika hilo kutoa fedha kwa njia ya mikopo nafuu na misaada kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya iliyopangwa kutekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa nyumba 10,000 za Watumishi wa Umma, kukuza mauzo ndani na nje ya nchi kupitia taasisi za fedha na sekta binafsi, pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tunguu – Makunduchi visiwani Zanzibar, yenye urefu wa km 48.
Aliitaja miradi mingine inayoombewa fedha kutoka Shirika hilo kuwa ni Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Songea mkoani Ruvuna, Mradi wa Maji Safi na salama wa Mafinga, mkoani Iringa na Ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Dawa na Vifaa Tiba, Chamazi, Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa OPEC FUND, Dkt. Alkhalifa Abdulhamid Saleh, aliahidi kuwa Mfuko wake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.
Alisema kuwa Mfuko huo umepanga pia kushirikiana na Tanzania kuisaidia sekta binafsi ili iweze kukua zaidi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji huo wa uchumi na maisha ya wananchi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhe. Nadhifa Kemikimba na viongozi kutoka idara mbalimbali za Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ujumbe kutoka Mfuko wa OPEC.