Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Ujerumani Kushirikiana Kuboresha Utamaduni
Apr 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Katja Keul katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali ya Tanzania pamoja na Shirikisho la Ujerumani zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika kuboresha Utamaduni na Malikale ili kuendelea kuhifadhi urithi wa historia ya nchi kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Katja Keul wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Katja Keul yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi Mulamula amesema kuwa Ujerumani imekuwa na msaada mkubwa katika maendeleo ya kijamii, kitamaduni, kielemu na kiuchumi. “Kwa sasa tunaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Ujerumani. ziara ya Mhe. Keul hapa nchini imelenga kuangalia namna gani tunaweza kuongeza ushirikiano katika masuala ya utamaduni na malikale ambapo katika kutimiza hilo tayari mkataba wa ushirikiano wa kuendeleza makumbusho yetu ya taifa umesaini jana,” amesema Balozi Mulamula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Katja Keul. Wengine pichani ni Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Regina Hess, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdalla Possi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Swahiba Mndeme pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Maafisa walioambatana na Mhe. Keul katika ziara yake hapa nchini.   

Nae Waziri Keul amesema kuwa Ujerumani na Tanzania zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano na lengo kuu ni kuongeza ushirikiano katika masuala ya utamaduni na malikale kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Katika kuhakikisha tunaongeza na kuboresha ushirikiano katika masuala ya utamaduni na malikale, tumesaini mkataba wa ushirikiano kati ya Makumbusho ya Taifa na Mfuko wa Utamaduni wa Ujerumani lengo likiwa ni kuhakikisha malikale na uhifadhi wa historia zinalindwa na kusaidia jamii kisayansi, kielimu, kiutamaduni na kiuchumi,” amesema Mhe. Keul 

Kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008, malikale hujumuisha rasilimali za urithi wa utamaduni zinazoshikika na zisizoshikika; zinazohamishika, na zisizohamishika, zilizo nchi kavu na majini ambazo zinadhihirisha mabadiliko ya kimaumbile, kifikra, zana, vyombo na mazingira aliyoishi na kutumia binadamu na zenye umri wa miaka mia moja (100). Malikale hizi zinajumuisha zana za mawe na chuma, vyombo vya usafiri, metali, miti na mifupa; visukuku vya binadamu, mimea na wanyama; michoro ya miambani; miji ya kihistoria, magofu ya majenzi.  

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi