Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Uganda Kushirikiana Kupeleka Umeme Vijiji Vya Mpakani
Jul 31, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_7960" align="aligncenter" width="750"] Mawaziri mbalimbali kutoka Serikali za Tanzania na Uganda wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkutano wao kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera hivi karibuni.[/caption]

Na:  Veronica Simba – Kagera

Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) wa kupeleka umeme kwenye Vijiji vya Mpakani mwa nchi hizo.

Hati ya Makubaliano hayo ilisainiwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga akiwakilisha Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania) na Waziri wa Nishati wa Uganda, Dk. Simon D’Ujanga, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa nchi hizo kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika mjini Bukoba, Mkoani Kagera.

Makubaliano ya msingi katika Hati iliyosainiwa ni utekelezaji wa Mradi wa kupeleka umeme kwenye vijiji vya Nangoma, katika eneo lililopo mpakani mwa Tanzania na Uganda na vijiji vingine vya maeneo hayo kwa kutokea upande wa Tanzania.

[caption id="attachment_7963" align="aligncenter" width="750"] Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka Serikali za Tanzania na Uganda (katikati), wakiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka nchi hizo, walioshiriki katika Mkutano unaohusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika hivi karibuni, mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera.[/caption]

Akifafanua zaidi kuhusu makubaliano husika, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, ambaye pia alishiriki Mkutano huo mkubwa, alisema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini kwa upande wa Tanzania (REA-Tanzania) utahusika katika kugharamia ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kufikisha umeme katika eneo la mpakani, umbali wa kilomita 0.8 kwa gharama ya Dola za Marekani 36,923.05.

Aidha, aliongeza kuwa, kwa upande wa Uganda, Wakala wa Nishati Vijijini wa nchi hiyo (REA-Uganda) utahusika kugharamia ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 umbali wa kilomita 7.5 kutoka eneo la mpakani hadi katika vijiji vya Bukwali Gamuli, Bushungulu, Nangoma, Omurushenye, Mizinda na Lukunyu kwa gharama ya Dola za Marekani 724,239.06.

[caption id="attachment_7964" align="aligncenter" width="825"] Balozi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Tanzania), Dk. Augustine Mahiga (Kulia) na Balozi wa Mambo ya Nje wa Uganda, Sam Kutesa (Kushoto), wakibadilishana Hati za Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) kupeleka umeme kwenye Vijiji vya Mpakani mwa nchi hizo, baada ya kutiliana saini hivi karibuni mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera. Katikati ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia Nishati wa Uganda, Dk. Simon D’Ujanga[/caption] [caption id="attachment_7965" align="aligncenter" width="811"] Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard kalemani (kulia), akichangia hoja wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika hivi karibuni mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na katikati ni Naibu Waziri, Tawala Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo.[/caption]

Alieleza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), litakuwa na jukumu la kuuza umeme kulingana na Mkataba wa kusambaza umeme utakaosainiwa kati yake na Shirika la Umeme la Uganda.

Vilevile, alisema kuwa, REA-Tanzania itashiriki katika kusaidia upatikanaji wa Mkandarasi atakayehusika na ujenzi wa Mradi kwa upande wa Uganda.

Katika Mkutano huo pia, masuala mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda, katika sekta ya nishati yalijadiliwa ambapo ilielezwa kuwa, mwaka 2014, Serikali hizo mbili zilisaini makubaliano (Bilateral Agreement) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kuzalisha umeme wa Murongo-Kikagati wa Megawati 14 kwa manufaa ya nchi zote mbili.

[caption id="attachment_7966" align="aligncenter" width="824"] Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati), akiwa katika Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika hivi karibuni mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera.[/caption] [caption id="attachment_7969" align="aligncenter" width="750"] Ujumbe wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoka Tanzania, wakifuatilia kwa makini Mkutano uliowakutanisha wao na wenzao kutoka Uganda (hawapo pichani) kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani uliofanyika hivi karibuni mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera.[/caption] [caption id="attachment_7972" align="aligncenter" width="750"] Wanasheria na wataalam wa masuala ya nishati kutoka Tanzania, wakijadiliana jambo, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda kuhusu ushirikiano katika masuala ya mpakani, kabla ya kusainiwa kwa Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) wa kupeleka umeme kwenye Vijiji vya Mpakani mwa nchi za Tanzania na Uganda.[/caption]

Mradi mwingine wa ushirikiano katika sekta ya nishati, uliojadiliwa katika Mkutano huo ni wa kuzalisha umeme wa Nsongezi wa Megawati 35, ambapo ilielezwa kuwa, Serikali za Tanzania na Uganda zina nia ya kutekeleza Mradi huo kwa kutumia chanzo cha maji ya Mto Kagera ambao upo mpakani mwa nchi hizo.

Wataalam wamependekeza kuwa, hatua muhimu za utekelezaji wa miradi kama vile kufanya Upembuzi yakinifu wa Mradi, upatikanaji wa Mshauri Mwelekezi na Mwendelezaji wa Mradi, zifanyike kwa Ubia, chini ya uongozi wa Serikali ya Tanzania na Uganda.

[caption id="attachment_7973" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani (wa tatu kutoka kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, anayeshughulikia Nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili kutoka kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam mbalimbali kutoka wizarani, REA na TANESCO walioshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani. Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera.[/caption] [caption id="attachment_7978" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka Serikali za Tanzania na Uganda, wakisalimiana nje ya Ukumbi wa ELCT-Bukoba mjini, kabla ya kuanza kwa Mkutano wao kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani.[/caption] [caption id="attachment_7979" align="aligncenter" width="931"] Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaack Kamwelwe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhandisi Hamadi Masauni, wakibadilishana mawazo nje ya Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kabla ya kushiriki kikao cha ndani ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani.[/caption]

Masuala mengine ya ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Uganda katika maeneo ya Mpakani, yaliyojadiliwa katika Mkutano huo wa Mawaziri ambao uliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Tanzania) ni kilimo na uvuvi, maji, ardhi pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.

Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka nchi hizo mbili wanaoshughulika na masuala ya ushirikiano katika maeneo ya Mpaka, uliofanyika Julai 28, mwaka huu mjini Bukoba.

   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi