Na Benny Mwaipaja, Washington DC
Tanzania na Misri ziko katika hatua ya mwisho ya majadiliano ya kuipatia ufumbuzi changamoto ya utozaji kodi mara mbili kwenye bidhaa zinazoingia au kutoka katika nchi hizo mbili ili kusisimua biashara na kukuza mauzo nje ya nchi yatakayoongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Dkt. Rania Al-Mashat, kando ya mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa- IMF, Jijini Washington DC, Marekani.
Bw. Tutuba alisema kuwa majadiliano ya wataalam wa masuala ya kodi kutoka pande zote mbili yanaendelea na kuahidi kuwa ndani ya kipindi cha miezi miwili yatakuwa yamekamilika na kuwashauri viongozi wa juu wa nchi kuhusu hatua zilizofikiwa ili kuondoa changamoto hiyo kwa lengo la kuboresha biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Misri.
Kuhusu uwekezaji na ukuzaji biashara, Bw. Tutuba alimhakikishia Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Misri, Dkt. Rania Al-Mashat, kwamba Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kutoa wito kwa kampuni na mashirika ya Misri kuja kuwekeza Tanzania.
Bw. Tutuba alisema kuwa ziara iliyofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, iliwezesha kupatikana kwa wawekezaji 120 ikiwemo kampuni ya kuzalisha vifaa vya umeme zikiwemo transfoma, ya Elsewedy Electric East Africa.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeahidi kuiunga mkono Misri kuandaa Mkutano wa 27 wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika nchini humo wenye lengo la kutafuta fedha, teknolojia na uwezeshaji kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi hususan katika nchi za Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Dkt. Ranai Al-Mashat alisema kuwa Misri ni mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo hivi sasa Kampuni ya Misri inajenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kutumia maji wa Julius Nyerere na kwamba masuala ya hifadhi ya mazingira ni muhimu yakatiliwa mkazo kwa pamoja.