Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania na India Zaahidi Kuendeleza Ushirikiano
Feb 20, 2026
Tanzania na India Zaahidi Kuendeleza Ushirikiano
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Emmanuel Nchimbi Akifanya Mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bashwadip Dey, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Emmanuel Nchimbi, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bashwadip Dey, Ikulu jijini Dar es Salaam Februari 20, 2026, ambapo pande zote zimeahidi kuendeleza na kuimarisha  uhusiano wa kirafiki na wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Mazungumzo hayo yamelenga kukuza ushirikiano katika sekta za afya, maji, elimu, biashara na uwekezaji pamoja na masuala ya ulinzi na usalama. Aidha, viongozi hao wameeleza dhamira ya kuendeleza mahusiano ya kihistoria yaliyodumu kwa zaidi ya nusu karne.

Tanzania na India zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu baada ya uhuru wa Tanzania, ambapo India ilifungua ubalozi wake mwaka 1961 na Tanzania kufungua ubalozi wake nchini India mwaka 1962. Mahusiano hayo yaliinuliwa hadi ngazi ya kimkakati mwaka 2023 kufuatia ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini India.

Katika ushirikiano wa maendeleo, India imechangia kwa kiasi kikubwa miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali pamoja na kuimarisha sekta ya afya kupitia utoaji wa huduma, mafunzo kwa wataalamu na usambazaji wa vifaa tiba.

Kwa upande wa biashara, India ni miongoni mwa washirika wakuu wa Tanzania, ikishika nafasi ya tatu duniani kwa kiwango cha biashara na nchi hiyo. Bidhaa kuu zinazouzwa na Tanzania kwenda India ni pamoja na korosho, karanga, mazao ya jamii ya kunde, vito na madini ya thamani, pamba, karafuu, chai, ngozi pamoja na mbao na bidhaa za mbao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi