Serikali ya Tanzania inalenga kuongeza uwekezaji katika sekta za kipaumbele ikiwemo sekta ya Elimu, Afya, na Kilimo cha kisasa kinachozingatia mabadiliko ya Tabia nchi ili kuchochea ukuaji wa Uchumi Endelevu na Kupunguza Umaskini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Tathmini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia (IDA20 Mid-Term Review) unaohusisha wakopaji, nchi Wahisani na Menejimenti ya Benki ya Dunia, unaofanyika kwa siku tatu, Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine utajikita kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa katika nchi zenye kipato cha chini kupitia fedha za mkopo na msaada zinazotolewa na Mfuko huo uliopo chini ya Benki ya Dunia.
Rais Mwinyi alisema kuwa, mfuko wa IDA umechangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo Mradi wa Nishati ya umeme vijijini wenye thamani ya dola za Marekani milioni 200, ambao umewezesha kufikia zaidi ya watanzania milioni 2.5 kupata nishati ya umeme, pamoja na dola za Marekani milioni 335, ambazo zimetumika katika uboreshaji na ujenzi wa vituo vya Afya na Madarasa.
“Tunatambua namna ambavyo mfuko wa IDA, umekua kielelezo kizuri cha Ufanisi kwa nchi zenye uchumi wa chini” Alisema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Aidha, Mhe. Rais Mwinyi, ameiomba Benki ya Dunia kupitia dirisha la IFC na IDA kuangalia namna ya kukopesha sekta binafsi ili kuwezesha Ushindani wa Biashara katika eneo huru la biashara Afrika hatua itakayochochea ongezeko la ajira kupitia ushirikiano wa kikanda na biashara.
Naye Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), amesema kuwa Kaulimbiu ya Mkutano huu wa IDA-20 ambayo ni Ukuaji Endelevu wa Uchumi, Kujenga Uthabiti, na Kusaidia Maendeleo ya Mtaji wa Watu, inalingana kikamilifu na vipaumbele vya Tanzania.
“Kujitolea kwa Serikali yetu katika kuboresha miundombinu, kuwekeza katika rasilimali watu, na kukuza utawala bora, kumechangia kwa kiasi kikubwa mwelekeo wetu wa maendeleo, na pia Uongozi wa Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, umepiga hatua kubwa katika kukuza ushirikishwaji na kujenga uthabiti kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia, Bw. Ajay Banga, amesema kuwa Kabla ya kufika mwaka 2030, Benki ya Dunia kupitia Mfuko wa IDA, itatoa kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 5 kwa ajili ya kufikisha umeme wa uhakika, nafuu, na mbadala kwa Waafrika zaidi ya milioni 100.
“Katika siku chache zijazo, tutakuwa na fursa ya kutafakari juu ya manufaa yaliyotokana na IDA na kwa pamoja, na pia tutapata fursa ya kutoa maoni juu ya utendaji kazi wake ili kuweza kufikia nchi za kipato cha chini kwa ukamilifu wenye maono ya ukuaji” alisema Bw. Banga.
Mkutano huo wa Siku tatu unawakutanisha zaidi ya wajumbe 300 kutoka nchi zinazonufaika na IDA, Viongozi wa Benki ya Dunia, pamoja na Wafadhili wanaochangia Fedha katika Mfuko huo wa IDA.