Ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia umewasili nchini hii leo 03 Agosti, 2021 kwa ziara maalum ya kutathimini na kufahamu mahitaji na vipaumbele vya Tanzania katika sekta ya afya kwa hospitali zilizopo nchini.
Hatua hiyo imetokana na Serikali ya Italia kutenga kiasi cha Euro 1,250,000 za msaada wenye manufaa kwa Tanzania hali iliyoufanya Ujumbe wa madaktari watatu kufanya ziara kuanzia tarehe 03 – 12 Agosti, 2021 ambapo ujumbe huo utakutana Uongozi wa Wizara ya Afya na kuainisha mahitaji na viapumbele vitakavyoweza kufadhiliwa kwa fedha hizo katika sekta ya afya.
Ujumbe huo unaongozwa na Dkt. Davide Bonechi aliyefuatana na Dkt. Giulia Dagliana pamoja na Dkt. Beatrice Borchi, ambao wote ni Madaktari kutoka Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani.
Tanzania imekuwa ikishirikiana na Italia katika miradi mbalimbali ya afya hapa nchini ambapo ushirikiano rasmi katika sekta ya afya ulianza mwaka 1968 kupitia Shirika la Madaktari wa Italia-CUAMM-Doctors with Africa. Kuanzia wakati huo, Serikali ya Italia imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya afya kama vile miradi ya kupambana na utapiamlo, afya ya watoto wachanga, afya ya uzazi na kupunguza maambizi ya virusi vya ukimwi.
Aidha, Serikali ya Italia imefadhili miradi ya usafi wa mazingira jijini Dodoma ambapo pia katika kuunga mkono jitihada za serikali katika utoaji wa huduma za afya, Serikali ya Italia imekuwa ya kwanza kufungua Kituo cha Tiba ya Mifupa na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza katika Hospitali ya St. Gaspar, Dodoma. Vituo hivyo, vinaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuboresha afya ya wananchi wa Tanzania hususan wakazi wa Dodoma.