Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kujiimarisha Zaidi Kidiplomasia - Majaliwa
Sep 04, 2024
Tanzania Kujiimarisha Zaidi Kidiplomasia - Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndungulile, ofisini kwa Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Septemba 4, 2024.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kujiimarisha kidiplomasia na itaongeza nguvu zaidi ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata fursa mbalimbali katika jumuiya za kimataifa.

 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikisha kuimarisha ushirikiano baina ya nchi washirika na sasa mafanikio yanaonekana.

 

"Rais wetu ameonesha nia njema katika kipindi chake cha miaka mitatu na nusu, amefanya kazi kubwa ya kujenga diplomasia na mahusiano katika sekta mbalimbali na nchi nyingi duniani."

 

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 4, 2024) alipokutana na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika (WHO), Dkt. Faustine Ndungulie, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.

 

Jitihada hizo za Serikali zimeiwezesha Tanzania kuendelea kupaa kidiplomasia na kuiwezesha nchi kupata viongozi wakubwa ndani ya Taasisi za kimataifa.

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndungulile, ofisini kwa Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Septemba 4, 2024.

"Tunaamini kazi kubwa tulizozifanya katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya kumpata Spika wa Umoja wa Mabunge Duniani haikuwa kazi ndogo, na tena tumepata Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika."

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumuunga mkono Mkurugenzi huyo katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.

 

"Wakati wote Waziri wa Afya atakuwa karibu nawe kuhakikisha kwamba sera zetu zinaenda sambamba na malengo ya WHO, kwa uwepo wako sisi lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba tunakuunga mkono kwa mipango yetu ya afya ndani ya nchi."

 

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndungulile amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuunga mkono na kufanya ushawishi wa kidiplomasia ili kufanikisha ushindi huo.

 

"Kwa upekee sana ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa katika kufanikisha ushindi huu kwa ushawishi wake kwenye jumuiya za kimataifa, pia nawashukuru viongozi wengine wa Serikali, Bunge na wadau wote."

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi