Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Finland Kushirikiana na Sekta ya TEHAMA
Mar 25, 2024
Tanzania, Finland Kushirikiana na Sekta ya TEHAMA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting kuhusu mashirikiano katika sekta ya TEHAMA.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Machi 25, 2024 jijini Dar es Salaam, ambapo pia yalimuhusisha Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland, Bw. Juhana Lehtinen na Mkurugenzi wa Nokia nchini Tanzania Amouneu Lopy.

Waziri Nape amesema kuwa ushirikiano baina ya Finland na Tanzania umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza Sekta ya TEHAMA nchini, ambapo amezungumzia Mradi wa TANZICT (2011-2016) uliotekelezwa baina ya Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Finland uliowezesha uandaaji wa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016.

Ameongeza kuwa, sera hiyo ilikuwa msingi wa kutengeneza sheria nzuri zilizowezesha kukua kwa matumizi ya TEHAMA nchini. Hivyo, hauwezi kuzungumzia mafanikio ya sekta ya TEHAMA bila kuitaja Finland.

Viongozi hao walizungumzia pia masuala ya usalama mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi, uchakataji wa taka za kielektroniki pamoja na kukuza matumizi ya vifaa janja vya kielektoniki kwa kuhakikisha vinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili matumizi ya TEHAMA yaende sambamba na uwekezaji unaofanyika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi