Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, AFASU Yasaini Makubaliano Kuwezesha na Kukuza Uwekezaji, Biashara na Utalii Nchini.
Oct 12, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na. Beatrice Sanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Geoffrey Mwambe pamoja na Raisi wa Jumuiya ya Muungano Kimataifa chini ya kundi la Afrika na Asia (Afro- Asian union (AFASU), Dkt. Hossam Darwish wametia saini hati ya makubaliano ya  kujumuika, kukuza na kuunda ushirikiano katika sekta ya uwekezaji (MoU)  wenye lengo la kuwezesha na kukuza uwekezaji, biashara na utalii nchini Tanzania .

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Jijini Dar es salaam, Mhe. Mwambe ameainisha maeneo ambayo Tanzania na ASAFU watashirikiana katika kuvutia maeneo ya uwekezaji kuwa ni pamoja na uwekezaji katika kilimo, Viwanda, Biashara ya Kielektroniki, Utalii, elimu pamoja na Uwekezaji katika ICT na uanzishaji wa elektroniki.

Mhe. Mwambe ameeleza kuwa kusainiwa kwa hati ya makubaliano kunaonyesha dhamira kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita  ya kushirikiana na wadau wote  duniani  na kuwaalika katika uwekezaji lakini pia kutumia fursa  ya kuaminika kama  serikali ya Tanzania  kuweza kuwaomba  Taasisi  na sekta binafsi waweze kutusemea  ili kushawishiana kuja kuwekeza Tanzania kwasababu ya mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa nchini.

“Serikali hii inaaminika  na mazingira ya uwekezaji Tanzania yameendelea kuboreshwa  na pia sisi  kwenye Nyanja za kimataifa  tafsiri yake ni kuwa tanzania inaendelea  kusifika kwenye  ubora wake wa mazingira ya uwekezaji”Amesema Mhe. Mwambe

Aidha, Mwambe amewashukuru wawekezaji hao na kuwahakikishia kuwa ofisi yake iko tayari kushirikiana nao kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wanafanikiwa, na kuwataka watanzania na Taasisi nyingine za serikali  kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kufanikiwa kuwekeza nchini.

“Nawashukuru sana AFASU, nawakaribisha sana na ninawaomba watanzania tuendelee kuwapa ushirikiano wote  pale ambapo wataitaji vibali, ardhi,  na idhini mbalimbali za serikali  ili waweze kutekeleza mradi wao  tutahakikisha kwamba tunasimamia hilo  kwahiyo tusingependa kuwakwamisha  kwa sababu hii inatupa sifa sisi na  inampa pia amani Mhe. Rais na kuendelea kujenga imani kubwa kwa  wawekezaji wa ndani na nje ya nchi

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya hiyo, Dkt. Hossam Darwish amesema Jumuiya ya AFASU wako tayari kutekeleza vipengele vyote ambavyo  vimo ndani ya makubaliano  hayo na watatekeleza kwa nguvu kubwa na  haswa kwa kuanza na sekta ya kilimo  ambapo ndani ya Jumuiya   wanao wajumbe ambao  ni  wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya kilimo   ambapo wameona maeneo ya kilimo na  wamevutiwa sana na fursa  hiyo ya kilimo hapa nchini  na hivyo  wanatoa ishara njema  kwamba wao watakuwa ni sehemu ya uwekezaji katika sekta hii ya kilimo  pamoja na sekta nyingine ambazo zitakuwa zimeainishwa katika makubaliano.

Dkt. Hossam ameongeza kuwa  kwa hatua ya kwanza na kwa haraka wataanza na mradi  wa chuo  cha  Kimataifa cha Kitanzania  cha mifumo ya kielektroniki ambacho kitakuwa na vitivo mbalimbali vya kimasomo  ya kielimu na wanaimani kwamba vitivo hivyo  vinaweza kwenda sambamba  na kile walichokiona kinahitajika ndani ya nchi yetu   ambapo shahada mbalimbali zitatolewa kupitia chuo hicho na kitaweza kuchukua wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za Afrika nakuhakikisha kuwa mfumo wa masomo utaweza kutoa wataalamu wa kutosha.

Amesema hatua nyingine itakayofuata ni mradi wa maonyesho ya biashara ambayo yatafanyika hapa nchini Tanzania ili kuweza kuchochea uwekezaji na pia jumuiya hiyo itajikita katika uwekezaji wa masuala ya utalii hususan katika ujenzi wa hoteli zenye hadhi kubwa na katika sekta ya afya watajikita katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha Dawa na vifaa Tiba .

Kwa upande mwingine, Dkt. Hossam amemshukuru Waziri wa Uwekezaji kwa  kuonesha uzalendo mkubwa kwa nchi yake ambapo amekuwa na juhudi kubwa sana  na kwa upande wake anamatumaini makubwa kuwa Tanzania itapiga hatua katika sekta hii ya uwekezaji kwa juhudi kubwa ambazo anazifanya Waziri wa Uwekezaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi