Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TANROADS Yakamilisha Matengenezo ya Barabara ya Morogoro - Iringa
Jul 18, 2023
TANROADS Yakamilisha Matengenezo ya Barabara ya Morogoro - Iringa
Muonekano wa Barabara ya Morogoro-Iringa, mara baada ya matengenezo yake kukamilika eneo la Iyovi.
Na Mwandishi Wetu

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kufanya ukarabati na maboresho ya barabara ya Morogoro kuelekea Iringa (Tanzam Highway) ili kunusuru barabara hiyo kukatika katika eneo hatarishi la Iyovi ambalo kingo za mto Ruaha zinakutana na tuta la barabara lenye mteremko na kona kali.

Hayo yameelezwa jana baada ya Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mussa Kaswahili kutembelea eneo hilo na kuzungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Meneja wa TANROADS wa mkoa huo Mhandisi, Alinanuswe L. Kyamba.

Mhandisi Kaswahili, alisema kuwa katika msimu wa mvua zilizoisha mwezi Aprili mwaka 2023, zilisababisha madhara katika eneo hilo baada ya maji ya mto Ruaha kujaa na kugonga tuta la barabara na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa na kupelekea barabara kutishia kukatika hali ambayo isingedhibitiwa mapema ingeweza kukwamisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika barabara hiyo ambayo inaunganisha Tanzania na nchi jirani za Zambia na Congo.

“Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Mtendaji Mkuu wa TANROADS ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Barabara ilitenga fedha za haraka kiasi cha shilingi milioni 480 kwa ajili ya ukarabati na maboresho ya kingo za barabara hiyo na baada ya taratibu zote ikampa kazi Mkandarasi mzawa wa kampuni ya CGI Construction Company Limited ambaye amekamilisha kazi kwa wakati na muda uliopangwa”, alieleza Mhandisi Kaswahili.

Alisisitiza kuwa barabara hiyo ni moja ya barabara zinazotumiwa na wasafirishaji wanaopokea mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, hivyo ni jicho la TANROADS, kwa ujumla inaangaliwa kwa ukaribu na inahudumiwa kama kipaumbele cha kwanza katika kila bajeti inayotengwa kila mwaka kwa Mkoa wa Morogoro na inapohitajika fedha za dharura hutengwa ili kuhakikisha barabara hiyo na nyingine zenye umuhimu kama hiyo zinakuwa salama na zinapika wakati wote pasipokuwa na changamoto yoyote.

Mhandisi Kaswahili aliongeza, “TANROADS tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kutenga fedha na kuzipeleka maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya maendeleo na matengenezo ya barabara, Rais hajawahi kuacha kutuletea fedha, wananchi wanapaswa kufahamu kuwa Serikali ipo makini inawajali, ipo pamoja na wao na ipo kwa ajili ya kutekeleza miradi kuhakikisha hawapati changamoto yoyote kwenye eneo la miundombinu hasa ya barabara”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi