Na Tiganya Vincent - RS Tabora
SERIKALI kupitia Shirika lake la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) itajenga Kituo kidogo (sub station) mpakani mwa Urambo na Kaliua na kingine kitajengwa unapokaribia kuingia Nguruka kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi wa wilaya hizo na maeneo jirani.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni kabla ya kuanza ziara yake ya siku moja mkoani humo kukagua miradi ya usambazaji umeme vijijini.
Alisema kuwa lengo la ujenzi wa vituo hivyo ni kurekebisha hali ya upatikanaji wa umeme na kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika ambao utawawezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji bila wasiwasi.
Katika hatua nyingine Waziri wa Nishati alisema Serikali itaendelea kuwatembelea Wakandarasi waliopewa jukumu la kujenga miundo mbinu ya kusambaza umeme vijiji chini ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu ili kuhakikisha wanakamilisha kazi kama walivyokubaliana katika mkataba.
Alisema wamewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha wanawasha walau vijiji vitatu kila wiki kwa ajili kuharakisha upelekaji wa umeme kwa wananchi waliopo maeneo ya vijijini.
Aidha alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni umebaini kuwepo na vijiji 1541 ambavyo vilikuwa havijaingizwa katika mradi huo hivyo vitaingizwa mwakani ili navyo viweze kuangashiwa umeme.
Waziri huyo wa Nishati aliagiza wananchi wapatiwe umeme katika maeneo yote ya vijiji ambayo tayari kuna miundombinu ya umeme inapita bila kusubiri Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu.
Akisoma taarifa ya Mkoa . Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Nathalis Linuma alisema kuwa katika REA III jumla ya vijiji 162 vitanufaika na huduma ya umeme kwa mzunguko wa kwanza.