Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TANAPA Yakabidhiwa Magari 14 Kutoka Mradi wa REGROW
Aug 29, 2020
Na Msemaji Mkuu

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu akizungumza jana Agosti 28, 2020 jijini Dodoma na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, Menejimenti ya Wizara pamoja na Waandishi wa Habari kabla hajakabidhi magari 14 yaliyotolewa chini ya mradi wa kusimamia maliasili na kuendeleza Utalii kanda ya kusini (REGROW). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi.

Na Jacquiline Mrisho

Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) imekabidhiwa magari 14 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 yanayolenga kuboresha utalii katika Hifadhi za Taifa zilizoko katika ukanda wa kusini za Ruaha, Udzungwa na Mikumi.

Fedha hizo ambazo ni mkopo wa masharti nafuu ni sehemu ya dola za marekani milioni 60 zilizotolewa na Benki ya Dunia ambayo kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, zinatekeleza mradi wa kusimamia maliasili na kuendeleza Utalii kanda ya kusini (REGROW).

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari 14 yaliyotolewa chini ya mradi wa kusimamia maliasili na kuendeleza Utalii kanda ya kusini (REGROW) aliyoyakabidhi TANAPA jana Agosti 28, 2020. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara.  

Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo jana jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alisema kuwa magari hayo ni awamu ya kwanza, ambapo magari mengine 9 yanatarajiwa kufika hivi karibuni kwa ajili ya hifadhi mpya ya Julius Nyerere.

Naibu Waziri Kanyasu alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa pili wa maendeleo ambapo moja kati ya vipaumbele vya kimkakati vinavyokuza uchumi wa nchi ni sekta ya utalii, hivyo lazima kuendelea kutatua changamoto katika sekta hiyo.

“Utalii unachangia takriban asilimia 17 ya Pato la Taifa hivyo kuletwa kwa magari haya katika Hifadhi za Taifa zilizoko kusini zikiwemo za Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Julius Nyerere kutaboresha hali ya utalii katika hifadhi hizo na kutaongeza mapato nchini”, alisema Kanyasu.

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi (Kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara  (kulia) pamoja na viongozi wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo baada ya kukabidhi magari hayo jana Agosti 28, 2020 jijini Dodoma.   

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi alisema kuwa fedha za mradi huo zitatumika katika jitihada za kukabiliana na tatizo la ujangili ikiwa ni moja wapo ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza utalii  na kuimarisha usimamizi katika maeneo ya kusini ili yaweze kujulikana kitaifa na kimataifa.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuthamini mchango wa utalii katika nchi yetu na kusaini mkopo huo ambao utakuwa chachu ya kuimarisha utalii nchini pia tunaishukuru Benki ya Dunia kwa kukubali kufadhili mradi huu”, alisema Dkt. Kijazi.   

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Dkt. Allan Kijazi (Kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara  (kulia) pamoja na baadhi ya watumishi wanaosimamia mradi huo. 

Nae, Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara   amefafanua kuwa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi ya Hifadhi za Taifa, Bodi ya Utalii, Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori, Tume ya Umwagiliaji na Bodi ya Bonde la Maji la Rufiji.

“Mradi huu unatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia malengo yake makuu yakiwemo ya kuimarisha usimamizi wa maliasili kwa kuboresha miundombinu, kuimarisha shughuli mbadala za kiuchumi kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi hizo za kusini pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji eneo la nje la Hifadhi ya Ruaha”, alisema Waitara.

Kupitia utekelezaji wa sehemu ya kwanza, TANAPA inaendelea na taratibu za manunuzi ya ujenzi wa barabara, nyumba za kulala wageni na viwanja vya ndege ndani ya hifadhi pia imepanga kununua magari madogo na mitambo ili kuwezesha kusimamia vizuri maeneo yaliyohifadhiwa na kuimarisha miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi