Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAKUKURU kubaini mamluki michuano ya Mei Mosi 2018
Apr 17, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_30455" align="aligncenter" width="1000"] Baadhi ya wachezaji wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakisikiliza kwa makini maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa kamati ya michuano ya Kombe la Mei Mosi katika kikao kilichofanyika jana kwenye uwanja wa Samora, yakiwa ni maandalizi ya michuano hiyo iliyoanza jana [/caption]

Na Bahati Mollel-TAA, Iringa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU), itafanya ukaguzi wa wachezaji wanaoshiriki kwenye michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa, ili kubaini wachezaji wasio waajiriwa wa serikali ‘mamluki’, kwa kuwa sio sheria kutumiwa kwa wachezaji hao.

Akizungumza jana na wachezaji waliowasili mkoani Iringa kwa ajili ya kushiriki kwenye michezo hiyo, Afisa kutoka Takukuru, Bw. Mweri Kilimali amesema endapo watabaini kuwepo kwa wachezaji hao watawachukulia hatua ikiwemo ya kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi na kuingizia serikali hasara.

“Hawa wachezaji wanakuwa wakitumia rasilimali za serikali kwani wanakuwa wamelipwa posho kutoka serikalini kutokana na taasisi au wizara iliyomsajili, hivyo wote waliohusika akiwemo Afisa Utumishi watachukuliwa sheria kutokana na kuihujumu serikali na watafungwa kutokana na kosa hilo, kwani wanakuwa wamekula njama ya kumsajili mtu ambaye sio mtumishi wa umma na kumlipa posho kutoka katika fungu la fedha za serikali,” amesema Bw. Kilimali.

[caption id="attachment_30456" align="aligncenter" width="1000"] Afisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Iringa, Bw. Mweri Kilimali (aliyesimama) jana akielezea kifungu namba 28 kinachohusiana na ubadhirifu wa mali za serikali kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano ya Kombe la Mei Mosi yanayofanyika katika uwanja wa Samora.[/caption]

Bw. Kilimali amewataka viongozi wote wa michezo walioambatana na timu zao kuhakikisha wanawasomea wachezaji kanuni hizo za mashindano na kuweka msisitizo kila wakati ili wasiende kinyume na kanuni hizo.

Pia wasidhubutu kufanya kosa la kukiuka na kutumia madaraka yao vibaya na kusajili wachezaji wasiokuwa waajiriwa halali wa serikali, kwa kuwa ni kosa lililopo chini ya kifungu namba 28 cha makosa ya ubadhirifu na watafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi kwa kuwa watakuwa wameiingizia serikali hasara.

Naye Katibu Mkuu wa Kamati ya michezo ya Mei Mosi, Bw. Award Safari amesema adhabu mbalimbali zitatolewa kwa watakaochezesha mamluki kwa mujibu wa kanuni za michezo hiyo namba 13.0 kipengele 13.1 ambapo kiongozi au viongozi watakaohusika kumsajili mamluki watafungiwa kwa kipindi cha miaka miwili, huku mchezaji husika ataondolewa katika kituo cha mashindano, na timu husika itapigwa faini ya sh. 500,000.

Bw. Award amesema adhabu nyingine ni timu husika iliyochezesha mamluki itanyang’anywa ushindi endapo itakuwa imeshinda, huku viongozi au kiongozi aliyehusika kusajili mamluki ataandikiwa barua na nakala yake itapelekwa kwa mwajiri wake, ikionesha udanganyifu aliofanya na kuiingizia ofisi yake hasara.

[caption id="attachment_30457" align="aligncenter" width="1000"] Katibu wa Mashindano ya Kombe la Mei Mosi, Bw. Award Safari (wa pili kushoto), jana akiongea na wanamichezo awapo pichani kwenye uwanja wa Samora akitoa maelezo mbalimbali ya kuhusiani na mashindano hayo, ambayo yameanza jana na ufunguzi utafanyika rasmi April 21, 2018.[/caption] [caption id="attachment_30458" align="aligncenter" width="1000"] Wachezaji wa timu ya Uchukuzi wakisikiliza maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa Kamati ya Michuano ya Kombe la Mei Mosi katika kikao kilichofanyika jana kwenye uwanja wa Samora, mkoani Iringa. Michuano hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 21, 2018 na Mkuu wa Mkoa Mhe. Amina Masenza.[/caption]

“Ili kudhibiti mamluki lazima kila mwanamichezo kuwa na kitambulisho chake halisi cha kazi, kadi ya bima ya afya, kadi ya mfuko wa jamii na hati ya malipo ya mshahara ya miezi miwili ya Februari na Machi 2018, na vitatumika kama vielelezo endapo mchezaji yeyote atalalamikiwa kuwa ni mamluki,” amesema Award.

Award amezitaja kanuni nyingine kuwa ni  pamoja na usajili ni lazima wachezaji wote wajaze fomu maalumu zitakazotolewa na Kamati ya mashindano itakayokuwa na majina na picha yake halali.

Aidha, kanuni ya ushindi utatambulika kwa pointi, magoli ya kufunga na kufungwa, na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, na endapo timu zitafungana kwa kila kitu basi utaratibu wa kurushwa shilingi utatumika.

Naye mjumbe wa Kamati ya michezo ya Mei Mosi, Bi. Joyce Benjamin amesisitiza wachezaji kuwa na nidhamu ndani na nje ya kiwanja , ikiwemo ya mavazi na kauli za staa kwa kuwa wachezaji wote ni watumishi wa umma hawapaswi kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

“Haitapendeza kumuona mtumishi wa umma ambaye tupo naye hapa katika michezo amevaa nguo fupi na za kubana na kuja nazo huku uwanjani au kutembea mitaani, pia kutoa kauli chafu kwa wachezaji au viongozi wa timu yake au pinzani au kwa waamuzi, hatutasita kumuandikia barua kali ya onyo na nakala kupelekwa kwa mwajiri wake ili amchukulie hatua zaidi za kinidhamu,” amesema Bi. Benjamin.                      

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi