Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taifa Litaendelea Kumkumbuka Lowassa
Feb 16, 2024
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Taifa litaendelea kumkumbuka Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa kwa rekodi kubwa ya usimamizi wa shughuli za Serikali ikiwemo usimamizi wa ujenzi wa shule za sekondari katika kila Kata.

 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 16, 2024) wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge, ambapo amesema ujenzi wa shule hizo uliwezesha watoto wengi waliofaulu elimu ya msingi kujiunga na elimu ya sekondari na alitilia mkazo suala la elimu na kupiga vita mimba kwa wanafunzi.

 

Amesema suala lingine ni kurasimisha biashara ya pikipiki (Bodaboda) kubeba abiria jambo ambao limesaidia vijana kupata ajira, kusimamia uanzishwaji wa SACCOS nchini pamoja na kubadili Vyuo vya Ualimu vya Mkwawa na Chang’ombe ili viwe vyuo vikuu vya ualimu.

 

Waziri Mkuu amesema Hayati Lowassa alihimiza ujenzi wa zahanati katika kila kijiji na ujenzi wa vituo vya afya katika kila Kata, alisimamia kikamilifu kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), alihamasisha  jamii ya wafugaji kupenda elimu kwa kuanzisha shule nyingi za sekondari katika maeneo yao.

 

Waziri Mkuu amesema kuwa licha ya hayo, kati ya mwaka 1990 na 2005, Hayati Lowassa aliwahi kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Mahakama, Masuala ya Bunge na Uratibu wa Maafa; Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

 

Pia, Waziri Mkuu amesema Hayati Lowasa alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Mazingira na Kuondoa Umaskini; na Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo. “Nafasi ambazo alizitumikia kwa weledi na ameacha alama kubwa kwa Taifa letu.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Hayati Edward Lowasa anatarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi Februari 17, 2024 Monduli mkoani Arusha. Hayati Lowassa alifariki Jumamosi, Februari 10, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi