Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TaBSA Yandaa Mafunzo ya Baseball kwa Walimu wa Shule za Sekondari Dodoma.
Aug 17, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Agness Moshi

Chama cha Mchezo wa Baseball Tanzania (TaBSA) kimeandaa mafunzo ya siku mbili yatakayofanyika Agosti 19 na 20 katika viwanja vya Shule za Sekondari mjini Dodoma.

Mafunzo hayo yatatolewa kwa lengo la kuitikia wito uliotolewa Februari 17, 2016 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa uliovitaka vyama vya michezo Nchini kujiimarisha katika Nyanja mbalimbali ikiwa pamoja na kuwaendeleza waalimu wazawa   kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa.

Taarifa iliyotolewa Jijini Dar es Salaam na Katibu mkuu wa TaBSA Bw.Alpherio Nchimbi imeeleza kuwa, Mafunzo hayo yataendeshwa na mtaalamu wa mchezo huo kutoka Japan kupitia Shirika la Maendeleo Kimataifa la Japan (JICA) Bw.Hiroki Iwasaki na yatafunguliwa rasmi   Agosti 19 na Mwenyekiti wa Kamati ya michezo ya Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni katibu tawala wa Mkoa huo.

Mafunzo hayo yatatolewa kwa nadharia na vitendo kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa timu imara ya mchezo huo kwa ngazi ya Taifa ambayo itakua ikishikiriki mashindano ya michezo hiyo ikiwa ni pamoja na mashindano ya Afrika Mashariki mwaka huu,Dunia kwa mwaka na 2018 na Olimpiki kwa mwaka 2020.

Aidha,Wahitimu wa mafunzo hayo watakabidhiwa vyeti pamoja na vifaa vya kufundishia mchezo huo  ili wasaidie kukuza uelewa kwa wanafunzi pamoja na wadau wa baseball hapa nchini.

Katika kuendeleza mchezo huo TaBSA imefanya juhudi mbalimbali za kukuza na kuendeleza mchezo huo ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa walimu wazawa ambapo hadi sasa wameshatoa mafunzo katika mikoa ya Mwanza,Kilimanjaro,Mbeya,na Ruvuma.

TaBSA imetoa wito kwa waalimu, wadau na wapenda michezo kwa ujumla mkoani Dodoma kuhudhuria ili waweze kuufahamu zaidi mchezo huo, pamoja na kupata ujuzi utakaowawezesha waalimu kuufundisha kwa ufanisi na weledi zaidi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi