Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete yaendelea Kuimarika
Jun 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Georgina Misama.

Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 26 katika kujenga na kuweka miundombinu  ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)

Akiongea katika kipindi cha TUNATEKELEZA, Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alisema kwamba takribani bilioni 13 zimetumika katika kuweka miundombinu ikiwemo mitambo ya kisasa pamoja na mashine muhimu.

“Tunao mtambo  maalumu wa kufanyia upasuaji wa Moyo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4, ni mtambo wa kisasa ambao unapatika katika hospitali kubwa duniani” alisema Prof. Janabi.

Akiongelea idadi ya wagonjwa wanaofika kupatiwa huduma katika hospitali hiyo Prof. Janabi alisema kuwa Taasisi hiyo inapokea wagonjwa 150 – 200 kwa siku wakitokea ndani pamoja na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati, baadhi ya wagonjwa hao ni watoto wadogo ambao wengi wana matatizo waliyozaliwa nayo.

Hospitali inahudumia Watanzania wote wanaohitaji huduma bila kujali uwezo wa kifedha wa mgonjwa kwani hata wasiomudu gharama za matibabu hupatiwa huduma sawa na wagonjwa wengine.

Baadhi ya huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwetea ni pamoja na upasuaji ambapo toka kuanzishwa kwake mpaka sasa wagonjwa 996 wameshafanyiwa upasuaji.

Prof. Janabi anasema kwamba mpaka sasa Taasisi hiyo imetibu wagonjwa zaidi ya 2000 na baadhi ya wagonjwa hao hupatiwa huduma ya kuwekewa betri kutokana na shida zao, ambapo betri wanazowekewa hudumu kwa miaka 10.

“Tunafanya kazi kwa kushirikiana na waatalamu kutoka Hospitali kubwa Duniani kama Israel, Marekani na Ulaya. Lakini pia tunaendelea kuzalisha wataalamu wa Moyo wa ndani ili tuweze kujenga uwezo zaidi wa kutoa huduma. Dhamira yetu ni kuifanya Taasisi kuwa kituo bora cha nchi nyingine kuja kujifunza” Anasema Prof. Janabi

Aidha, Prof. Janabi ametoa rai kwa watanzania kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara, kwani katika utafiti waliofanya hivi karibuni, waligundua kwamba 46% ya watu waligundulika kuwa na shinikizo la damu bila wenyewe kujitambua.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete ilifunguliwa rasmi Septemba 4, 2015 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mrisho Jakaya Kikwete na kupewa jina lake. Kabla ya hapo ilikuwa Idara inayoshughulikia magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi