Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa ya Ziara ya Makamu wa Rais Uswisi na Sweden
Jun 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango hivi karibuni amefanya ziara katika mataifa mawili ya Uswisi pamoja na Sweden kwa lengo la kushiriki Mikutano ya Kimataifa pamoja na kuongeza ushirikiano baina  ya Tanzania na mataifa hayo na mengine yalioshiriki mikutano hiyo.

Akiwa nchini Uswisi tarehe 22 – 26 Mei, 2022, Makamu wa Rais alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika   mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani uliofanyika Davos nchini Uswisi.   

Jukwaa la Uchumi Duniani huwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Wakuu wa Taasisi na Makampuni mbalimbali duniani pamoja na Wafanyabiashara.

Kando na mkutano huo, Makamu wa Rais akiwa nchini Uswisi alifanya mikutano mbalimbali ya ushirikiano na viongozi waliohudhuria Jukwaa hilo la Uchumi ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Malkia Maxima wa Uholanzi ambaye ni mwakilishi maaalum  wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ujumuishwaji wa mifumo ya fedha kwa maendeleo. Pia Makamu wa Rais alifanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Czech, (CHEK) Jozef Fikela kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa yote mawili.

Nchini Sweden Makamu wa Rais alifanya ziara tarehe 31 Mei hadi Juni 4 2022. Tarehe 1 Juni 2022 alitembelea makao makuu ya kampuni ya utengenezaji wa magari ya Scania iliopo Stockholm nchini Sweden. Makamu wa Rais akashiriki mazungumzo na Mkurugenzi wa Teknolojia Endelevu ya Utengenezaji Magari wa Kampuni ya Scania Jonas Strömberg pamoja na mkuu wa teknolojia endelevu ya usafirishaji wa kampuni ya Scania, Fredrik Wijkander, mazungumzo yaliolenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Kampuni hiyo.

Tarehe 2  Makamu wa Rais akahutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 ambao ulikua na dhumuni la  kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na  janga la Uviko 19.

Tarehe 3 Juni, 2022 Makamu wa Rais akafanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mheshimiwa Ann Linde kwa lengo la kuongeza ushirikiano baina ya mataifa haya mawili.

Pia Makamu wa Rais alipata wasaa wa kutembelea na kuweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Sweden na mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania, Hayati Olofu Palme.

Aidha, Makamu wa Rais akiwa nchini Sweden alifanya mazungumzo na viongozi wa Watanzania waishio Sweden, aliwasikiliza changamoto zao na kuahidi kuzifanyika kazi pamoja na kuwasihi diaspora hao kuendelea kutoa mchango wao katika diplomasia ya uchumi wakiwa huko ughaibuni.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi