Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini jioni ya leo kuelekea Addis Ababa, Ethiopia ambapo atahudhuria Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameagwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali.
Katika Mkutano huo wa siku mbili kuanzia tarehe 03-hadi 04 Julai-2017, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan atamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo.
Kabla ya ufunguzi rasmi, Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Baraza la Utendaji linalowashirikisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Kamati ya Uwakilishi wa Kudumu inayowahusisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje kutoka nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali utafunguliwa rasmi tarehe 03-Julai-2017 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa, Ethiopia na utajikita katika kujadili masuala mbalimbali yanayohusu umoja huo.
Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na taarifa kuhusu Maboresho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na maboresho ya kitaasisi katika AU na hali ya Ulinzi na Usalama katika bara la Afrika.
Kuhusu hali ya ulinzi na usalama katika Bara la Afrika majadiliano ya Viongozi hao yatajikita zaidi kwenye nchi za Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na Libya. Aidha, majadiliano hayo pia yatagusa hali ya usalama kwenye baadhi ya nchi ambazo ziliathiriwa na kundi la Boko Haram za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.
Mkutano huo 29 wa AU, unatarajiwa kuhuduhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.
Mkutano huo 29 wa AU utakaofanyika Jijini Addis Ababa, Ethiopia utaongozwa na Mheshimiwa Alpha Conde Rais wa Jamhuri ya Guinea ambaye ndiye Mwenyekiti wa AU.
Kauli Mbiu ya Mkutano huo ni Kuimarisha Mgawanyiko wa Idadi ya Watu Kupitia Uwekezaji katika Vijana (Harnessing Demographic Divident Through Investments in the Youth)
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ADDIS ABABA- ETHIOPIA.