Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Awashukuru Watanzania kwa Maombi Dhidi ya Ugonjwa wa Corona
Jun 07, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_53026" align="aligncenter" width="633"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati alipokuwa akiendesha Harambee ya Papo kwa papo kwa ajili ya upanuzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Bikira Maria Imaculata Chamwino Ikulu mkoani Dodoma leo tarehe 7 Juni 2020. Katika Harambee hiyo jumla ya Shilingi Milioni 17 zilipatikana pamoja na mifuko 76 ya Saruji na Mhe. Rais Magufuli alichanga peke yake kiasi cha Shilingi Milioni 10.[/caption]

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru Viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa kuitikia wito wa kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Mhe. Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo tarehe 07 Juni, 2020 alipokaribishwa kuwasalimu Waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino Mkoani Dodoma baada ya kuhudhuria Misa Takatifu ya Sikukuu ya Utatu Mtakatifu iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Paulo Mapalala.

Mhe. Rais Magufuli amesema Mwenyezi Mungu amejibu maombi ya Watanzania ambao wamesali, wamefanya toba na kufunga, na matokeo yake ni kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yamepungua, na wananchi wanaendelea na maisha yao huku wakichapa kazi za uzalishaji mali, tofauti na ilivyodhaniwa kuwa ugonjwa huo ungesababisha madhara makubwa.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa makini dhidi ya mbinu zozote zinazoweza kufanywa kuwaambukiza ugonjwa huo ama magonjwa mengine, huku wakimshukuru na kumtumaini Mwenyezi Mungu aliye muweza wa yote.

Akiwa Kanisani hapo Mhe. Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia upanuzi wa Kanisa hilo na kufanikiwa kuchangisha shilingi Milioni 17,229,000/- (ikiwemo shilingi Milioni 10 aliyochangia yeye mwenyewe) na mifuko 76 ya saruji, na ametaka upanuzi wa Kanisa hilo uanze kesho.

  Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU Chamwino 07 Juni, 2020

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi