Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassana amesema ataunda kikosi kazi maalum ambacho kitafanya kazi ya kuchunguza matatizo mbalimbali yanayowakuta wafugaji kote ili Serikali iweze kuwasaidia kutatua matatizo hayo ikiwemo kukosekana kwa maeneo rasmi yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya malisho ya mifugo nchini.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Chama cha Wafugaji nchini ambao walimpelekea kilio chao kuhusu matatizo na manyanyaso wanayopata wakiwa katika shughuli zao za ufugaji Ikulu, Dar es Salaam.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema amepokea mapendekezo ya wafugaji hao na Serikali itafanyia kazi ili kuondoa hali ya sintofahamu inayowakuta wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini kwa sasa.
Makamu wa Rais pia amewataka wafugaji waache kutumika kama mtaji wa kisiasa kwani kufanya hivyo kutarudisha nyuma jitihada za kuimarisha na kuboresha shughuli zao nchini.
Amesema ili kujua kwa kina hali ilivyo Serikali itaunda kikosi kazi hicho ambacho kitatembelea maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo yenye migogoro ili kuhakikisha suluhu ya matatizo hayo ikiwemo migogoro kati ya wafugani na wakulima inapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania Magembe Makoye akisoma taarifa ya wafugaji hao kwa Makamu wa Rais ameeleza kuwa kukosekana kwa maeneo ya malisho ndio chanzo kikubwa chaa kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, hifadhi za taifa na wawekezaji nchini.
Amesema kama Serikali za mikoa na wilaya kote nchini zitaiga mfano wa mikoa Katavi na Ruvuma ambayo imeshatenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji migogoro kama hivyo nchini itakuwa ni historia.
Katibu huyo ameiomba Serikali kuwapatia mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji ili nao waweze kufanya shughuli zao za ufugaji katika maeneo hayo.
Ameeleza kuwa kama Serikali itawapatia maeneo maalum kwa ajili ya kufuga sekta ya mifugo nchini itawavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi ambao wataanzisha viwanda vitakavyotumia malighafi zinazotokana na mifugo kwa sababu hakutakuwa ni migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ikulu- Dar es Salaam.
15-June-2017.