Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma.
May 26, 2017
Na Msemaji Mkuu

Tanzania na Uganda Zasaini Mkataba wa Bomba la Mafuta la Hoima-Tanga Mjini Kampala

Kampala, Uganda

26 Mei, 2017

Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania lenye urefu wa Kilometa 1,443, uliokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola bilioni 3 nukta 55, mjini Kampala Uganda, leo.

Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi na Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni.

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya Marais wa Nchi hizo mbili, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni, kutia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Hafla ya kutia saini Mkataba huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Kampala, Uganda imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakurugenzi na Viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.

Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba wa mradi huo Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania inathamini uwepo wa mradi huo na imejipanga kuhakikisha unatekelezwa kwa mafanikio.

Nae Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda Mhe. Irene Muloni amesema Uganda imeamua kusafirisha mafuta yake kupitia bandari ya Tanga kutokana na Tanzania kukidhi matakwa yenye faida za kiuchumi katika utekelezaji wa mradi huo na kwamba utazinufaisha nchi zote mbili.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga Tanzania, unatarajia kusisimua uchumi wa nchi hizo mbili na katika mchakato wa ujenzi wake zaidi ya watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira.

Hivi Karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliuelezea mradi huo kuwa ni mkubwa kwakuwa Uganda imegundua shehena kubwa ya mafuta katika eneo la Hoima kiasi cha mapipa bilioni 6 na laki 5 na kwamba Tanzania inatarajia pia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambayo yatapitishwa katika bomba  hilo hilo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi