Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma.
May 23, 2017
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Shirikisho la Taifa la Utengenezaji wa Mitambo ya Viwanda la China (China National Machinery Industry Federation - CNMIF) kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawapa ushirikiano wa kutosha katika mpango wao wa kuwekeza katika uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda na kilimo hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Mei, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa CNMIF na Mbunge wa Bunge la Wananchi wa China Bw. Zhan Xin.

Mhe. Dkt. Magufuli amesema Tanzania imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts kati ya 1,500 na 1,800 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia Megawatts 10,000 na kwamba ili kufikia malengo hayo wawekezaji wanakaribishwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo kama vile gesi, makaa ya mawe na jua.

“Kwa hiyo Ndg. Zhang Xin kawaambie wawekezaji wenzako wa China waje Tanzania, nchini zetu ni ndugu na marafiki wa miaka mingi, itakuwa jambo jema wakija kuunga mkono juhudi zetu za kujenga viwanda kwa kuzalisha umeme mwingi na pia kushiriki katika miradi mingine ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Balozi wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Malika Berak ambapo viongozi hao wamezungumzia utekelezaji wa mambo mbalimbali ya ushirikiano pamoja na miradi ya maendeleo iliyotokana na makubaliano ya Mkutano wa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa uliofanyika hivi karibuni.

Viongozi wengine ambao leo wamekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli ni Kaimu Balozi wa Uturuki hapa nchini Bw. Yunus Belet na Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Korea Bw. Songwon Shin.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

23 Mei, 2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi