Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Oct 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

 Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ukanda wa Maziwa Makuu (7th Ordinary Summit of International Conference of the Great Lakes Region Heads of State and Government).

Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) umefanyika leo tarehe 19 Oktoba, 2017 mjini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo. Mkutano huo umetanguliwa na Mikutano ya Awali katika ngazi ya Wataalamu wa Masuala ya Fedha, Wakuu wa Vyombo vya Usalama, Wakuu wa Majeshi, Waratibu wa Nchi (ICGLR National Coordinators) pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje.

Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo akimwakilisha Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano huo.

Mkutano huu umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali na Wawakilishi wao kutoka nchi za Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudani, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.

Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kupitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na usalama katika eneo la Nchi za Maziwa Makuu hasa katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudani Kusini. Ajenda zingine zilikuwa ni pamoja na kupokea taarifa ya Michango ya nchi wanachama.

Kuhusu hali ya usalama katika Nchi za Maziwa Makuu kwa ujumla iliripotiwa kuwa inaendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa katika nchi za eneo hilo isipokuwa nchini DRC ambapo sasa hivi operesheni zinazoendelea kufanywa na Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC- MONUSCO (FIB) dhidi ya vikundi vya waasi vya ndani ya DRC na vile vinavyotoka nje ya nchi hiyo.

Mkutano huu ulifuatiwa na Mkutano wa Nane Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mpango wa Amani na Usalama katika Maziwa Makuu (8th Regional Oversight Mechanism for the Peace, Security and Cooperation Framework of the DRC and the Region).

Taasisi zingine za kimataifa zilizoalikwa kwenye Mkutano hii ni pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo ujumbe wake uliongozwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi