Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Apr 12, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kuhakikisha Wajasiriamali wenye vitambulisho hawatozwi ushuru wala tozo nyingine yoyote inayohusiana na biashara wanazofanya na kwamba kama kuna sheria ndogo zilizokuwa zikihalalisha utozaji huo zibadilishwe.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 12 Aprili, 2019 baada ya wananchi wa Migori Wilayani Iringa na Mtera Wilayani Mpwapwa kuusimamisha msafara wake uliokuwa ukielekea Dodoma na kumueleza kuwa wamekuwa wakitozwa kiwango kikubwa cha ushuru licha ya kuwa na vitambulisho vya Wajasiriamali.

Akiwa Migori wauzaji wadogo wa samaki wamedai Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imemweka mzabuni ambaye amekuwa akiwatoza ushuru wa zaidi ya shilingi 5,000 kwa kila tenga la samaki lenye uzito wa kilo 10, na kufuatia malalamiko ya Wajasiriamali hao (wengi wao wakiwa akina Mama) ameiagiza Halmashauri hiyo kuvunja mkataba na mzabuni aliyepewa kazi ya kukusanya ushuru wa halmashauri hiyo na kuhakikisha sheria ndogo inayotumiwa kukusanya ushuru huo inarekebishwa.

Akiwa Mtera, Mhe. Rais Magufuli amemtaka mzabuni anayekusanya ushuru kwa niaba ya halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kumrejeshea fedha zake kiasi cha shilingi 4,000 Mjasiriamali Leticia Mgonafivi baada ya Mjasiriamali huyo kudai ametozwa ushuru huo hapo jana licha ya kuvaa kitambulisho cha Mjasiriamali alichokilipia shilingi 20,000/-.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero nyingine za wananchi waliosimamisha msafara wake ambapo akiwa Migori Wilayani Iringa ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Migori ili kutatua changamoto ya matibabu inayoikabili kata ya Migori yenye wakazi 18,000.

Mbunge wa Jimbo la Ismani Mhe. William Lukuvi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kutatua tatizo la maji katika eneo la Migori baada ya kutekeleza mradi uliogharimu shilingi Bilioni 1 na Milioni 383 na pia ameshukuru kwa Serikali kutoa shilingi Bilioni 1 na Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Migori kwa kuacha uvuvi haramu na pia amewashauri wakulima wa eneo hilo na maeneo jirani kulima mazao yanayostahimili ukame badala ya kung’ang’ania kulima mahindi ambayo yamekauka kabla ya kukomaa kutokana na uchache wa mvua.

Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la maabara la Shule ya Msingi Chipogolo na ameagiza shule hiyo ipelekewe umeme.

Pia amemuagiza Diwani wa kata ya Mtera Mhe. Amoni Kodi kuandika kibao cha kuyatambulisha majengo yaliyoachwana mkandarasi wa barabara ya Iringa –Dodoma kuwa Kituo cha Afya cha Mtera na amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo kuhakikisha kituo hicho kinapelekewa watumishi na kinaanza kutoa huduma.

Mapema kabla ya kuondoka Mjini Iringa kuelekea Dodoma Mhe. Rais Magufuli amewaalika katika chai ya asubuhi viongozi wa Mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Ali Hapi, na katika salamu zake amewapongeza kwa umoja walionao katika kushughulikia kero za wananchi na kuhimiza maendeleo.

Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mhe. Ali Hapi kukifuatilia kiwanda cha karatasi cha SPM Mgololo kama kinafanya kazi kama ilivyotarajiwa ikiwemo jukumu kuu la kuzalisha karatasi.

Mhe. Rais Magufuli amewasili Mkoani Dodoma baada ya kumaliza ziara yake katika Mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Njombe na Iringa iliyoanza tarehe 02 Aprili, 2019.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dodoma

12 Aprili, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi