Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Jan 11, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Januari, 2019 amekutana na Mwenyekiti wa kampuni ya Bharti Airtel Bw. Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.

Baada ya mazungumzo hayo Bw. Sunil Mittal amesema kampuni yake imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 na hivyo kupunguza hisa zilizokuwazi kimilikiwa na Bharti Airtel kutoka asilimia 60 hadi asilimia 51.

Bw. Sunil Mittal ameongeza kuwa mazungumzo kati ya kampuni yake na Serikali ya Tanzania  yanakwenda vizuri na kwamba kampuni ya Bharti Airtel imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa katika masuala yaliyokuwa yakijadiliwa yenye lengo la kuiimarisha kampuni ya Airtel, kuleta manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo ambapo pamoja na kuongeza hisa za Serikali katika umiliki wa Airtel Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa gawio kwa Serikali ya Tanzania mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika hivi karibuni.

“Masuala mengine ya kumalizia mazungumzo haya yataendelea leo ilikumalizia,  lakini jambo zuri ni kuwa sasa wamekubali kutoa gawio kwa Serikali ambapo kwa muda wa miaka minane hadi kumi tulikuwa hatujapata gawio, kiasi cha asilimia za gawio nacho watajadili leo, kwahiyo mimi naona huu ni mwanga mzuri wa kwenda mbele kati ya kampuni ya Bharti Airtel na Serikali ya Tanzania pamoja na kampuni zingine” amesema Mhe. RaisMagufuli.

Kwa upande wa Tanzania timu ya majadiliano na kampuni ya Bharti Airtel inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

11 Januari, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi