Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Jun 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza Mawaziri Wawili wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu kwenda mkoani Mara haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kwenda kutatua changamoto zinazokabili sekta ya afya na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi hao.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo kijijini Butiama kwa viongozi wa mkoa wa Mara katika majumuisho yake ya ziara ya kikazi ya siku Tatu mkoani humo.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema ni muhimu kwa mawaziri hao kufika mkoani Mara mapema kwenda kutembelea maeneo husika na kutafutia ufumbuzi wa changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wananchi hao kwa muda mrefu sasa.

Ameeleza kuwa katika ziara yake mkoani Mara wananchi wamelalamikia sana kuhusu migogoro ya ardhi kati  ya kijiji na kijiji na kusuasua kwa utoaji wa  huduma za afya kwa wananchi na baadhi ya hospitali kukosa fedha kutoka Serikali jambo ambalo litapatiwa ufumbuzi na Waziri husika pindi watakapotembea maeneo husika.

Kuhusu hali ya ulinzi na usalama, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amepongeza jitihada zilizofanywa na Kamati za Ulinzi na Usalama ya Mkoa na za wilaya katika mkoa wa Mara katika kuhakikisha hali ya amani na utulivu inaimarishwa na kuendelea kudumishwa.

Ameeleza kuwa uimarishaji wa hali ya ulinzi na usalama kutasaidia kwa kiasi kikubwa mkoa wa Mara na wananchi wake kujikita zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali na kiongezea kipato kwa ajili ya familia zao.

Amesema miaka ya nyuma mkoa wa Mara ulikuwa unakabiliwa na matukio mbalimbali ya kihalifu lakini kwa sasa hali ni shwari na viongozi lazima wafanye kazi ili kuhakikisha hali hiyo inadumu kwa miaka mingi.

Makamu wa Rais pia amewataka viongozi katika ngazi mbalimbali wadumishe ushirikiano katika utendaji wao wa kazi ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa haraka.

Ameonya watendaji waache tabia ya kukaa maofisi bali wawatembelee wananchi katika maeneo yao  na kuzungumza nao ili kujua matatizo yanayowakabili na kuyatafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Mara Dkt Charles Mlingwa amemshukuru Makamu wa Rais kwa kufanya ziara ya kikazi mkoani humo na amemuahidi kuwa maelekezo na maagizo aliyoyatoa yeye pamoja na watendaji wa wilaya zote za mkoa wa Mara watayatekeleza kwa uhakika.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amemaliza ziara ya kikazi ya Siku Tatu mkoani Mara ambapo ametembelea wilaya za Butiama, Musoma Mjini, Tarime na ambapo amekagua, kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali na pamoja na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.

Akiwa njia kuelekea mkoani Mwanza kwa njia ya barabara, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisalimia wananchi wa mji wa Bunda walijitokeza kwa wingi barabarani na kuwaahidi kuwa ahadi zote zilizotolewa kipindi cha kampeni mwaka 2015 zitatekelezwa na Serikali ya awamu ya Tano ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za msingi katika maeneo yao.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais wa

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Butiama- Mara.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi