[caption id="attachment_34576" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe kuhusu barabara ya juu ya TAZARA wakati alipokagua hatua za mwisho za ujenzi wa barabara hiyo jijini Dar es salaam Agosti 29, 2018. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda.[/caption]
FLYOVER YA TAZARA IMEKAMILIKA KWA ASILIMIA 98 - MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesemaujenzi wa barabara ya juu katika eneo la Tazara umekamilika kwa asilimia 98 na itafunguliwa Oktoba mwaka huu na Rais Dkt. John Magufuli.
Mradi wa barabara ya juu (Mfugale flyover) chini ya ufadhili wa Serikali ya Japani, unalengo la kupunguza msongamano wa magari katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 29 ,2018) baada ya kukagua ujenzi wa mradi huowa barabara ya juu katika eneo la Tazara jijini Dar Es Salaam.
Waziri Mkuu amesema ameridhishwa kazi ya umaliziaji wa mradi huo inayoendelea kwenye hilo.
“Mradi utapunguza muda wa usafiri katika barabara ya Nyerere hususani kwa wananchi wanaotoka katikati ya jiji kwenda uwanja wa ndege na wanaotoka Buguruni, Temeke.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi Mkoa wa Dar Es Salaam watafute eneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo ili waweze kuondoka kandokando ya barabara hizo za juu zinazojengwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya kukagua ujenzi wa barabara za juu (interchange) eneo la Ubungo, katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma, eneo la Ubungo jijini Dar Es Salaam.
Amesema ni vema wafanyabiashara hao wakaondolewa na kutafutiwa eneo lingine ili kulinda usalama wao kutokana na kazi za ujenzi zinazoendelea kwenye maeneo hayo. Pia amewataka viongozi hao wawaelekeze wananchi maeneo watakapowahamishia wafanyabiashara hao ili waweze kwenda kununua bidhaa.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema mradi huo nao unalengo la kupunguza msongamano wa magari kwa kutenganisha njia za barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma ili kuwa na ngazi mbili juu ya barabara za sasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema ujenzi wa mradi wa barabara ya juu katika eneo la Tanzara (Mfugale flyover) unagharimu sh. bilioni 100.52 na unajengwa na kampuni ya Sumitomo Mitsui ya nchini Japan.
Amesema mradi huo umezingatia jinsi ya kuwezesha muunganiko wa mfumo wa usafiri jijini Dar Es Salaam na ule wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili, tatu na ya nne. “Tumeacha eneo la mita 12 katikati ya barabara kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 28, 2018.