Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa Kuhusu Uchaguzi wa Marudio Ukerere na Babati Mjini
Oct 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

Idara ya Habari-NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili na kata 26 za Tanzania Bara.

Majimbo hayo ni pamoja na Jimbo la Babati Mjini lililopo Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara na Jimbo la Ukerewe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza

Akisoma taarifa kwa umma Jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi) Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salum Mbarouk amesema kwamba uchaguzi huo utafanyika sambamba na uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro na Serengeti pamoja na kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.

“Nafasi hizo wazi zimetokana na waliokuwa Wabunge wa Majimbo hayo Bwana. Joseph Michael Mkundi (Ukerewe) na Bi. Pauline Philipo Gekul (Babati Mjini) kujiuzulu kutoka kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),” alisema Jaji Mbarouk.

Alifafanua kwamba Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Majimbo hayo mawili.

“Uchaguzi huu mdogo katika Majimbo ya Babati Mjini na Ukerewe utafanyika sambamba na uchaguzi katika Majimbo ya Serengeti, Simanjiro pamoja na Kata 21 zilizotangazwa awali….,” alisema.

Akisoma ratiba ya uchaguzi huo, Jaji Mbarouk amesema “fomu za uteuzi  wa  wagombea zitatolewa kati ya  tarehe 28 Oktoba hadi 3 Novemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 3 Novemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 4 Novemba  hadi tarehe 1 Desemba mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 2 Desemba, mwaka huu”.

Ametoa wito kwa wadua wa uchaguzi “Tunapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo”.

Katika hatua nyingine, Jaji Mbarouk amesema Tume imepokea taarifa kutoka kwa waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 26 za Tanzania Bara.

Aliongeza kuwa kwa  kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa taarifa kwa Umma kuhusu uwepo wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Majimbo ya Babati Mjini na Ukerewe   pamoja na Udiwani katika Kata Ishirini na Sita (26) za Tanzania Bara.

Majina ya Halmashauri na Kata zenye uchaguzi kwenye mabano ni kama ifuatavyo, Halmashauri ya Wilaya ya Temeke (Mtoni), Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (Mnyamani), Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa (Salanka), Halmashauri ya Wilaya ya Magu (Kabila), Halmashauri ya Misungwi (Sumbugu, Buhingo), Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe (Bukiko), Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (Miteja, Kivinje, Singino, Somanga na Mitole).

Nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Songea (Matarawe, Ruvuma), Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa (Mtipwili), Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (Magange, Ring’wani, Rung’abure, Natta na Rigicha), Halmashauri ya Mji wa Babati (Maisaka), Halmashauri ya Wilaya ya Meru (Nkoanekoli), na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti (Salale).

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi