Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAA yakusanya Bil. 98.1 za mapato kwa mwaka 2016/17
Jul 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mamlaka  ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imekusanya sh. Bil 98,140,621,387.54 kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya mapato kwa mwaka 2016/2017, imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela wakati akisoma taarifa fupi ya uendeshaji wa viwanja vya ndege vinavyosimamiwa na serikali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge iliyofanya ziara kwenye Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB1) na kituo cha Zimamoto cha kiwanja hicho.

Bw. Mayongela amesema chanzo kikubwa cha mapato ni tozo ya Huduma za abiria, ambacho kimekuwa kikiongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 zilikusanywa Tsh. Bil. 66.5; wakati kwa mwaka zimekusanywa 2015/16 Bil. 67.3 na mwaka 2014/2015 zimekusanywa Tsh. Bil. 51.4.

[caption id="attachment_33343" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa (aliyesimama) akieleza jambo fulani kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) hivi karibuni. Katikati ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe Suleiman Kakoso na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Richard Mayongela.[/caption]

Amesema pia TAA imekuwa ikikusanya mapato kutoka vyanzo vingine vya mapato ambapo kwa mwaka 2016/2017 imekusanya Bil. 31.6 ambazo zimeongezeka kutoka Tsh. Bil. 20.3 kuanzia mwaka 2012/2013 hadi 2014/2015.

Bw. Mayongela amesema pamoja na kukusanya mapato mengi bado TAA imekuwa ikipewa kiasi kidogo cha asilimia 40 ambacho kwa pamoja hakitoshelezi kwa matumizi mbalimbali yakiwemo ya gharama za uendeshaji ambazo zinaongezeka kwa kasi.

“Mapato yanayozalishwa na TAA yameongezeka kutoka sh. Bil 3.9 mwaka 1999/2000 hadi kufikia sh. Bil. 98.140 katika mwaka wa fedha 2016/2017, lakini kwa kuwekewa wigo tumerejeshewa asilimia 40 tu, ambazo hazitoshelezi kutokana na gharama za uendeshaji kupanda kwa kasi na kusababisha kuzorota kwa baadhi ya huduma katika viwanja tunavyosimamia,” amesema Bw. Mayongela.

        [caption id="attachment_33344" align="aligncenter" width="1000"] Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama) akiikaribisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye Jengo la Watu Mashuhuri (VIP) walipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) hivi karibuni. Katikati ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Suleiman Kakoso na kushoto ni Naibu Waziri, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa.[/caption]

Bw. Mayongela ameiomba kamati ya Miundombinu kuwasilisha maombi ya TAA katika Bunge kurejeshewa fedha za tozo za abiria kwa asilimia 100, ambazo zamani zilikuwa zikisaidia katika kuboresha miundombinu ya viwanja mbalimbali kwa kuwa baadhi ya viwanja havizalishi na vinavyozalisha havizidi vitano kati ya 58 vilivyopo.

Akizungumzia hali ya biashara katika viwanja vya ndege Bw. Mayongela amesema idadi ya safari za ndege imeongezeka kwa asilimia 136 kutoka jumla ya safari 62,221 mwaka 1999/2000 na kufikia safari 147,057 mwaka 2016/2017, ambapo ongezeko hilo ni kutokana na kuongezeka kwa mashirika mapya ya ndege na mengine kuongeza idadi ya safari.

Mbali na safari za ndege pia idadi ya wasafiri wa ndege wameongezeka kwa asilimia 301 kutoka jumla ya abiria 846,906 mwaka 1999/2000 hadi kufikia 3,393,006 mwaka 2016/2017 na ongezeko hilo limechangia kukua kwa shughuli za kiuchumi, hali kadhalika tani za mizigo zimeongezeka kwa asilimia 21 kutoka tani 16,463 mwaka 1999/2000 hadi 19,995 mwaka 2016/2017.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Suleiman Kakoso ameipongeza TAA kwa kufanya kazi nzuri ya kukusanya mapato mengi na kuongeza abiria, lakini amewataka wasibweteke na wafanye kazi kwa bidii kwa kuwa wamekuwa na washindani hususan Kenya ambao sasa wanafikisha abiria milioni tano kwa mwaka.

[caption id="attachment_33346" align="aligncenter" width="1000"] Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe Suleiman Kakoso (wa tatu kulia), wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (mwenye kipaza sauti) akielezea magari ya zimamoto na uokoaji, ambayo yapo kwenye Kituo cha Zimamoto cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakati walipotembelea kituo hicho hivi karibuni.[/caption]

Hatahivyo, amemuomba Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa kushirikiana na Waziri wa Wizara ya Fedha ili kurudisha asilimia 100 ya mapato yanayotoka TAA ili waweze kujiendesha.

“Nakuomba Mhe. Waziri ukashirikiane na Waziri wa Fedha muone ni namna gani mnaweza kurudisha kwa TAA hiyo asilimia 100 ambazo zipo kisheria zinazopelekwa serikalini, kwani viwanja vya ndege ndio vinavyokuza uchumi wa nchi, angalia majirani zetu Kenya wanaweza kwa kuwa wameachiwa kila mapato wanayatumia kwa matumizi ya uendeshaji,” amesema Mhe. Kakoso.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mhe. Kwandikwa amesema lengo la serikali ni kufanya maboresho katika taasisi zake, lakini ameahidi kuwasilisha suala la kurejeshewa asilimia 100 ili waweze kujiendesha kwa kuwa wanachangia uchumi wa nchi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi