Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kampuni ya StarMedia ambayo ina ubia na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) itatoa Bilioni tatu(3)kwa TBC kama ruzuku kwa mwaka 2018 kutokana na kufanyika mabadiliko ya Bodi ya StarMedia ambayo sasa Mwenyekiti wake ni Mkurugenzi Mkuu wa TBC.
Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo leo Mjini Dodoma wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari alipokuwa akijibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusiana na kampuni ya Ubia ya StarMedia ikiwa ni pamoja na mapungufu ya vifaa vya shilingi Bilioni 34.4 vyenye uchakavu wa dola za kimarekani Milioni 30.11 isivyo halali na kampuni ya StarMedia kutochangia gharama ya mtaji USD 650,000.
“Udhaifu katika maamuzi ya wawakilishi wetu kwenye kampuni ya ubia ya StarMedia ambao ulijitokeza dhahiri mwaka 2014 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TBC aliyepita, ambaye wakati huohuo alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya StarMedia aligomea kusaini hesabu za kampuni hiyo za mwaka 2014 kwa hoja kuwa baadhi ya hoja zilikosa uthibitisho na toka hapo akajiuzulu uenyekiti na kuwaachia Wachina kuongoza kampuni,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Amesema, suluhisho la changamoto haikuwa kujiuzulu kwa Mkurugenzi huyo bali kufanya maamuzi na kusimamia utekelezaji wake.
Aidha, amesema baada ya majadiliano ya muda mrefu na Startimes Group ambapo pia Dkt. Mwakyembe alishiriki na hatimaye kukubali taarifa ya CAG na mapendekezo yake yote, ikiwa ni pamoja na kuipa mara moja bodi ya Wakurugenzi madaraka stahili na hivyo kuruhusu uwazi wa kutosha katika uendeshaji wa kampuni pamoja na kuiruhusu TBC na wataalam wake kuingia kwenye mifumo ya TEHAMA ya uendeshaji wa kampuni hiyo ya ubia na kuleta uwiano upande wa wafanyakazi na viongozi wa kampuni hiyo ya pamoja.
Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa majibu ya hoja ya uchakavu wa Teknolojia na Karakana za SIDO, ambapo amesema, Wizara imetambua mapema kuwa, karakana saba za SIDO zilizoko katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Iringa, Shinyanga, Kigoma, Mbeya na Lindi zinazotengeneza teknolojia kwa ajili ya miradi ya wajasiriamali wadogo zimechakaa na kupitwa na wakati kwa sababu zina zaidi ya miaka 30.
"Kwa kutambua hilo, Wizara katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 imetenga jumla ya shilingi bilioni 5 ili kuanza kuzifanyia maboresho ya karakana hizo," alisema Mwijage.
Vile vile amesema, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya maendeleo kwa SIDO mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 SIDO ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 14.1 ikilinganishwa na mwaka 2016/2017 ambapo SIDO ilikuwa imetengewa shilingi bilioni 8.55 na mwaka 2018/2019 SIDO imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 26.8.
Mwijage ameongeza kuwa, Serikali itazidi kuipa uwezo SIDO ili iweze kufikisha huduma katika sekta kadri mapato ya Serikali yatakavyoruhusu.
Katika mfululizo wa Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kufafanua utekelezaji wa hoja mbalimbali za CAG, Jumatatu ijayo itakuwa zamu ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo.