Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Songwe Airport Yadhibiti Ugonjwa wa Ebola.
Jun 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_2845" align="aligncenter" width="750"] Afisa Afya Bw. Peter Alfred (katikati) akikagua hati ya kusafiria ya Bw. Paluku Ngahngondi (kushoto) Mkongo anayeishi Zambia kabla ya kupanda ndege ya Fastjet kuja Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Afya Bi. Shukrani Nkonjeka akiwa kwenye mashine maalum inayompima kila abiria anayepita mbele yake kwa kupiga picha na kutoa mlio wa endapo anajoto kali la mwili.[/caption]

Na Mwandishi wetu- TAA.

Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA) chafunga mashine maalum na ya kisasa ili kubaini abiria wenye dalili za ugonjwa wa Ebola.

Afisa Afya wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura Mkoa wa Songwe, Peter Alfred ameyasema hayo jana kiwanjani hapo ambapo wameweka kambi kwa ajili ya kuwabaini wagonjwa hao.

“Tumefunga mashine ya kisasa  ambayo abiria akipita umbali wa mita tano hadi 10 inampiga picha na kuonesha joto alilonalo mwilini na endapo atakuwa na joto la nyuzijoto 37.5 mashine hiyo itatoa mlio wa kengele,” alifafanua Alfred.

[caption id="attachment_2846" align="aligncenter" width="750"] Bi. Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya akimpa maelezo kuhusiana na ugonjwa wa Ebola mmoja wa wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), Bw. Fred Martin (kushoto).[/caption]

Amesema kuwa abiria atakayekuwa na joto hilo, atachukuliwa na kupelekwa eneo maalum lililotengwa umbali wa mita 300 kutoka eneo la kiwanja cha ndege na baadaye kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mbali na kuangaliwa kwa abiria wenye joto kali la mwili, pia hukagua na kupata maelezo binafsi kwa kujaza fomu maalum kwa abiria wote wanaopita kwenye kiwanja hicho wakitokea kwenye nchi za Kongo, Guinea, Sierra Leone, Mali, Nigeria, Liberia, Senegal, Marekani na Hispania kutokana na nchi hizo kuwa na historia ya kukumbwa na ugonjwa huo.

“Tangu zoezi hili limeanza, mara baada ya kupatikana kwa taarifa za ugonjwa huo kuwepo nchini Kongo, bado hatujapata mgonjwa mwenye dalili hizo na tunaendelea kuudhibiti kwani hapa ni njia kuu kwa abiria wanaotoka Kongo,” amesema Alfred.

[caption id="attachment_2848" align="aligncenter" width="750"] Madereva wa taxi wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), wakipokea vipeperushi vyenye maelezo mbalimbali yanayohusu ugonjwa hatari wa ebola kutoka kwa Afisa Afya, Bi. Shukrani Nkonjeka.[/caption]

Alfred amesema ugonjwa wa Ebola unasababishwa na virusi vya Ebola vinavyoingia mwilini mwa binadamu na wanyama kupitia puani, masikioni na machoni, na huambukiza kwa kugusa majimaji ya mwili toka kwa mtu aliyeambukizwa virusi hivyo, yakiwemo matapishi, damu, jasho, mkojo, machozi, kamasi na mate.

Aidha, binadamu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa au kuosha maiti ya aliyefariki kwa ugonjwa huo au kugusa shuka, godoro, nguo na blanketi lililotumika na mgonjwa. Pia kwa kuchomwa  sindano au vifaa visivyo safi na salama vilivyotumiwa na mgonjwa wa Ebola au kula matunda yaliyoliwa nusu na wanyama na kugusa mizoga au kula wanyama pori kama nyani, sokwe na popo.

[caption id="attachment_2851" align="aligncenter" width="750"] Bi Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya akiwapa maelezo yanayohusiana na ugonjwa hatari wa Ebola madereva wa taxi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA).[/caption]

Vile vile amesema dalili za ugonjwa huu zinaanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21 baada ya kupata maambukizi, ambapo mgonjwa hupata homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, misuli na viungo, vipele mwilini, kuvia damu chini ya ngozi, kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni, kuharisha na kutapika kunakoweza kuambatana na damu.

Alfred amesema ugonjwa huu hauna tiba maalum wala chanjo, lakini mgonjwa hupatiwa tiba saidizi kulingana na dalili alizonazo kama vile kushusha homa na maumivu, kuongezewa damu na maji mwilini na tiba lishe.

Wananchi wanaweza kujikinga na ebola kwa kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono au kukumbatiana, kuepuka kugusa majimaji yaliyotoka mwilini mwa mgonjwa wa Ebola au kuosha maiti, kuacha kutumia godoro, shuka na nguo za mgonjwa wa ebola pamoja na kuwahi haraka kituo cha kutolea huduma za afya endapo wataona dalili za ugonjwa huo.

 

 

 

 

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi