Hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuongeza mvuto kwa biashara ya mifugo na mazao yake nje ya nchi, zimeendelea kuzaa matunda ambapo mazao hayo yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/2021 hadi tani 13,745.38 mwaka 2024/2025.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amezungumza hayo jana Mei 06, 2025 jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO mbele ya waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
“Tani hizo zinafikisha jumla ya tani 40,635 zilizouzwa nje ya nchi kwa thamani ya shilingi 414,378,447,756 kwa muda wa miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita tangu kuingia kwake madarakani”, amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Ameeleza hatua zilizochukuliwa na Tanzania ili kukidhi masharti ya biashara ya mifugo na mazao yake kulingana na matakwa ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) kuwa ni uchanjaji mifugo ambapo serikali katika kuimarisha afya za mifugo inatarajia kuanza kampeni ya chanjo ya kitaifa hivi karibuni.
“Serikali inatarajia kuzindua Kampeni ya Chanjo ya Mifugo Kitaifa kati ya mwezi Mei hadi Juni, 2025 ambapo jumla ya dozi 19,099,100 za chanjo ya Homa ya Mapafu ya Ngombe (CBPP) zimenunuliwa na zinatarajia kuchanja jumla ya ng’ombe 19,099,100; jumla ya dozi 17,224,200 za chanjo ya Sotoka ya Mbuzi na Kondoo kwa ajili ya kuchanja mbuzi na kondoo 17,224,200; na dozi 40,000,000 za Chanjo ya ugonjwa wa kideri/mdondo (ND), ndui na mafua ya kuku kwa ajili ya kuchanja kuku wa asili 40,000,000”, amesema Waziri Kijaji.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kununua jumla ya hereni za kidijitali 36,323,300 kwa ajili ya utambuzi wa ng’ombe 19,099,100, mbuzi na kondoo 17,224,200 watakaochanjwa ambapo lengo kuu la utambuzi wa mifugo ni Kukidhi matakwa ya soko la kikanda na kimataifa linalohitaji kila mnyama na mazao yake kuwa na alama ya utambuzi pamoja na kumwezesha mfugaji kupata mikopo na bima.
Akizungumza kuhusu uvuvi, Mhe. Dkt. Kijaji amesema kuwa, katika kuimarisha usimamizi, uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi ikiwemo mazalia na makulia ya samaki, Serikali ya Awamu ya Sita katika mwaka wa fedha 2024/2025 imenunua ndege nyuki moja yenye thamani ya shilingi 259, 600, 000 ambayo imeunganishwa na mfumo wa ufuatiliaji wa wavuvi.
Ndege nyuki hiyo inatajwa kwamba itaongeza ufanisi katika kusimamia rasilimali za uvuvi kwa kupunguza gharama za doria na muda wa kukusanya taarifa na matukio katika maeneo ya uvuvi nchini.