Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ihakikishe kuwa mapato yatokanayo na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanatengwa na yanatumika katika sekta husika kulingana na miongozo iliyopo ili kuboresha sekta hizo.
“Ofisi ya Rais (TAMISEMI) hakikisheni mnasimamia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 unaozitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga mapato ya ndani yatokanayo na tozo mbalimbali kwenye mazao ya kilimo (asilimia 20), mifugo (asilimia 15) na uvuvi (asilimia 5) zinarudi na kutumika kuboresha sekta hizo ikiwa pamoja na uendelezaji wa mazao ya kimkakati,” alisema.
Alitoa wito huo jana (Alhamisi, Agosti 3, 2023) wakati akizungumza na wadau na washiriki mara baada ya kukagua mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Ili kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo, Waziri Mkuu aliwataka wadau wa sekta hizo wazitumie taasisi za fedha zilizopo nchini kupata mikopo itakayowasaidia kuongeza tija na kuendeleza biashara zao.
“Taasisi za fedha zimefungua dirisha kwa ajili yenu, wanataka wawasikie. Hakuna maendeleo bila kukopa, lakini ni lazima vigezo na masharti vizingatiwe. Unapotaka kufanya maendeleo ukakosa mtaji, nenda kakope lakini ukikopa mwisho wake lazima urejeshe ili na wengine waweze kukopa,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za fedha ili ziweze kushusha riba kwenye mikopo wanayotoa na kuongeza fursa kwa wajasiriamali nchini ili wapate mikopo na kuendeleza shughuli zao ziweze kuwa na tija. “Nimefurahi sana kukuta baadhi yao wameshusha riba mpaka asilimia tisa. Ni matumaini yangu watashuka zaidi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana na wizara husika kuhakikisha vijana wanapatiwa maeneo ya mashamba, mafunzo na kuwatafutia wadau watakaowasaidia kupata mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na masoko ya uhakika.
“Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa mshirikiane na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika maeneo yenu kuhakikisha mnatenga maeneo ili vijana wanaopata mafunzo ya BBT (mpango wa kuwawezesha vijana kulima, kufuga na kuvua samaki kibiashara) wakute yako tayari. Tunataka hawa vijana wakitoka kwenye mafunzo, wakute maeneo yako tayari na waanze kazi mara moja,” alisisitiza.