Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Siku ya Haki za Binadamu Kuadhimishwa Jumamosi
Oct 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na.Jovina Bujulu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itaadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Afrika kwa kufanya kongamano katika makao makuu ya tume hiyo, Jijini Dar es salaam, tarehe 21, mwezi huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa tume ,Francis Nzuki alisema kuwa kongamano hilo litawashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya haki za wafanyakazi ambapo watawasilisha na kujadili  mada mbalimbali .

“Mada zinazotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa ni pamoja na ‘Uchumi wa Viwanda na Haki za Wafanyakazi Tanzania’, ‘Matarajio na Changamoto za Mkakati Mpya wa Viwanda’ na  ‘Ulinzi wa Haki za Wafanyakazi Tanzania: Nadharia na Vitendo’ alisema Nzuki.

Aidha aliongeza kusema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu iliyotolewa na Umoja wa Afrika inasema “Kuimarisha mchango wa Vijana katika Kutekeleza Mpango Kazi wa Miaka kumi ya Haki za Bunadamu na Watu Afrika”

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli za Tanzania ya viwanda, tume imetangaza kauli mbiu inayosema “Uchumi wa Viwanda  na Haki za Wafanyakazi nchini Tanzania”.

Akizungumzia sababu nyingine za kuchagua kaulimbiu hiyo Nzuki alisema kuwa ni mkakati wa serikali wa kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali hasa viwanda ikiwa ni pamoja na  hofu ya athari za kukua kwa viwanda na biashara kwa haki za wafanyakazi.

“Sababu nyingine ni mchango wa wadau katika kuhakikisha kwamba serikali inalinda haki za wafanyakazi na  wawekezaji , na ambapo wafanyabiashara watatakiwa kuheshimu haki za wafanyakazi na waathirika wa uvunjifu  wa haki za binadamu wanapata nafuu inayostahili” aliongeza Nzuki.

Aidha katika siku hiyo itafanyika  tathmini kupitia majadiliano, kama sheria za kazi zinazotekelezwa na wawekezaji zina kidhi haja, na kuwa na mkakati wa pamoja wa kulinda na  kuheshimu mfumo wa utoaji nafuu kwa waathirika wa uvunjifu wa haki za binadamu.

Tume ya Haki za Binadamu ilianzishwa mwaka 2000 chini ya Ibara 129 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), kwa lengo la kulinda haki za binadamu.

Tanzania iliridhia Mkataba wa Haki za Binadamu uliopitishwa  na Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) mwaka 1984,na kuanza kutumika mwaka 1986. Mkataba huu unatambua haki za mtu mmoja mmoja,watu, ambapo unazingatia haki na wajibu na baadhi ya haki za kiuchumi, kijamii na kiraia.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi