Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sifa ya Tanzania Duniani ni Umoja na Mshikamano – JPM
Oct 26, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha tunu ya umoja na mshikamano iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili na kamwe wasikubali kuibomoa iwe kwa dini au kabila.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akishirikiana kukata utepe na
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally (aliyekuwa mgeni
rasmi) pamoja na viongozi wengine, wakati wa ufunguzi wa rasmi wa
msikiti wa Chamwino, uliofanyika leo Oktoba 25, 2020 jijini Dodoma.

Akizungumza leo (Jumatatu, Oktoba 26, 2020) wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wakati  akizindua msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Rais Magufuli alisema kuwa  msikiti huo utumike kuwaweka pamoja kama ndugu, pia ukawe fundisho kwa wana Chamwino na watanzania katika kuwa wamoja na kutambua kuwa wana wajibu wa kumtanguliza Mungu katika  maisha yote.

“Msikiti huu ukatoe mafunzo yatakayojenga umoja wa watanzania, ukaguse na mioyo yao ya kutekeleza maandiko matakatifu yaliyopo kwenye Quran na yakajenge umoja ndani ya watanzania wote,” alisisitiza.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akishirikiana pamoja na
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally (aliyekuwa mgeni
rasmi) kufungua kitambaa kwenye jiwe la msingi, wakati wa ufunguzi wa
rasmi wa msikiti wa Chamwino, uliofanyika leo Oktoba 25, 2020 jijini
Dodoma.

Aliongeza “ishara hii mliyoionyesha leo ni ya kipekee duniani kote, upendo huu na umoja huu ni wa maajabu sana, tuendelee kushikamana”

Aidha, Rais Magufuli aliwakumbusha watanzania kwenda kupiga kura  Oktoba 28 mwaka  huu kulingana na utashi wa mioyo yao kwa kuchangua viongozi watakaoweka mbele maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charls Mbuge alisema kuwa msikiti huo wenye ofisi ya Mufti umejengwa kwa gharama ya shilingi  milioni 319.28 umekamilika kwa asilimia 100.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameungana na viongozi
wengine kupokea dua iliyokuwa ikisomwa na  Mufti wa Tanzania, Sheikh
Abubakar Zubeir Bin Ally (aliyekuwa mgeni rasmi) katika ufunguzi rasmi
wa msikiti wa Chamwino, uliofanyika leo Oktoba 25, 2020 jijini Dodoma.

"Endapo msikiti huu ungejengwa na mkandarasi basi ungetumia shilingi  milioni 439.43, na umekamilika kwa asilimia 100 na tumeujenga kwa mwezi mmoja na siku 28 tu."

Aidha, Meja Jenerali Mbuge, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuifanya JKT kuwa karibu na wananchi na kuahidi  kuendelea kutekeleza maagizo pamoja na majukumu  yao kwa ufanisi.

Naye Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea msikiti wenye hadhi na sambamba na uamuzi wake wa kurudisha mali za waislamu zilizopotea.

"Umekuwa kiongozi  mwenye kipaji cha kupenda viongozi wa dini na mwenye kumtanguliza Mungu katika Kila jambo. Vitabu vya Mungu  vinasema anayefanyia wema mlipeni na kama hamna cha kumlipa muombeeni."

Aidha, Mufti Zuberi alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu, huku wakiendelea kuliombea taifa hata baada ya Uchanguzi Mkuu kumalizika.

Itakumbukwa kuwa Agosti 23, 2020, Rais Magufuli aliendesha  harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti  wa Chamwino katika  misa takatifu  ya uzinduzi wa  Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Immaculata   Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, ambapo shilingi millioni 25.6  zilipatikana.

Mwisho

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi