Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akijaribu kuendesha trekta alilokabidhi kwa kituo cha utafiti wa kilimo TARI Ilonga jana ikiwa ni mkakati wa wizara kuviwezesha vituo hivyo kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kwenye mashamba yake.Jumla ya matrekta saba yamenunuliwa na wizara kupitia TARI mwaka huu . Katika kuhakikisha Tanzania inajitosheleza na uwepo wa wataalam bora wa kilimo serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 70 kuboresha miundombinu ya vyuo 14 vya mafunzo ya kilimo (MATI) nchini. Kauli hiyo imetolewa jana (14.09.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa vyuo vya mafunzo ya Kilimo Ilonga na TARI Ilonga wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro. Alibainisha kuwa uwepo wa mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vya mafunzo ya kilimo na vituo vyake yatawezesha kufanya mapinduzi katika kupata teknolojia bora na mafunzo ya kilimo kuwezesha ukuaji wa sekta ya kilimo. “ Katika mwaka huu wa fedha tumepanga kutumia shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kukarabati vyuo vyetu vya kilimo vya serikali ikiwemo kuweka miundombinu wezeshi ya kufundishia ,vifaa vya kufundishia na kuongeza wakufunzi na wanafunzi” alisema Kusaya Kusaya akiwa katika ziara hiyo ya kikazi alibainisha mikakati saba ya wizara ya kilimo katika kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inakuwa na tija na kuchangia ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa watanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akimwagilia mche wa muembe aliopanda jana alipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Ilonga na kuagiza vyuo vyote vya umma nchini kujitegemea kibiashara kwa kuwa na mashamba darasa.
Alisema serikali inahitaji kuwafundisha vijana wawe tayari kuwa maafisa ugani bora watakaofundisha ujuzi pamoja na tekenolojia bora katika kwa vyuo vya umma na binasfi.
Mkakati wa kwanza wa wizara Kusaya alisema ni kuhakikisha inakabiliana na upungufu wa wakufunzi 247 wanaotakiwa kwenye vyuo vyote 14 vya serikali kwa kuanzisha mpango wa kutumia wahitimu wa vyuo vikuu vya kilimo kufanya mazoezi ya kazi ( interns) ili kupunguza tatizo.
Pili wizara ya kilimo itaanzisha kanzi data ya wahitimu wa mafunzo ya kilimo kwenye vyuo vya umma na binafsi ili kufahamu wapi walipo wanafunzi na kazi gani wanafanya ,lengo serikali iweze kujua namna gani ya kuwaunganisha na vikundi vya uzalishaji mali kupitia taaluma yao ya kilimo.
Tatu, wizara itaanzisha vituo atamizi kwa ajili ya wanafunzi waliohitimu mafunzo ya kilimo kuwawezesha vijana kutumia elimu yao kuanzisha shughuli za kilimo biashara kivitendo ili waweze kujitegemea na kusaidia kufundisha vijana wengine vijijini na mijini.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitazama teknolojia ya kisasa ya kutumia chupa kuzalisha mbegu za bora za migomba wakati alipotembelea kituo cha utafiti TARI Dakawa wilaya ya Mvomelo jana. Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa wanafunzi watakabidhiwa vitalu nyumba (green haouse) kupitia usimamizi wa wakufunzi ili wazalishe mazao kwa kutumia elimu waliyoipata na kuwa vituo hivi vitasaidia kuwafanya wanafunzi wengi kuwa mahili kwenye uzalishaji mazao na kufundisha wakulima wengine. “ Uwepo wa vituo atamizi utasaidia wakulima wengi kupata mafunzo kwa vitendo toka kwa vijana wahitimu wa kilimo watakaowezeshwa na wizara kufanya kilimo biashara hali itakayoongeza ajira na tija katika uzalishaji wa mazao nchini” alisisitiza Kusaya. Kusaya alitaja mkakati wa nne ni kuhakikisha vyuo vya mafunzo ya kilimo vinatoa teknolojia ya kisasa kwa kutumia mtandao ndio maana mwisho mwa mwezi Agosti alikabidhi kompyuta 05 kwa vyuo vyote 29 vya kilimo vya umma na binafsi na kuwa lengo kila chuo kitapatiwa kompyuta 30 ifikapo mwisho mwa mwaka huu. ”Tunataka kuwa na mfumo wa kufundisha kielektoni (e-learning) ili kuunganisha vyuo vyote kutumia vifaa vya kompyuta na kuleta mapinduzi katika fani ya kilimo” alielekeza Kusaya. Mkakati wa tano wa wizara ni kuhakikisha vyuo vyote vinatumia ardhi iliyopo kuzalisha mali na kufundisha wanafunzi kupitia mashamba darasa na kuwa serikali itatoa trekta moja kwa kila chuo cha mafunzo ya kilimo cha serikali ili kuweka mazingira rafiki na waweze kujiendesha kibishara.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akitazama mche wa mchikichi wakati alipokagua kitalu cha miche bora katika kituo cha utafiti TARI Ilonga wilaya ya Kilosa jana.Kituo hicho kimefanikiwa kuotesha miche 600,000 ambayo itagawiwa kwa wakulima wa mkoa wa morogoro lengo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula. “ Vile vyuo vinavyojihusisha mfano na uzalishaji wa mpunga au ngano tutawapelekea zana zinazoendana na mafunzo wanayotoa kwa wanafunzi ili waongeze tija na uzalishaji na hatimaye wapate mapato ya kujitegemea kiuchumi” alisisitiza Kusaya. Sita, wizara ya kilimo itatoa magari kwa vyuo vyote 14 vya mafunzo ya kilimo vya serikali na kugawa pikipiki tatu ili kurahisisha upatikanaji wa usafiri na utoaji huduma. “ Tayari tumepeleka pikipiki sita katika vyuo Inyara Mbeya, Igurusi Mbeya na Ukirigulu Mwanza kila kimoja pikipiki mbili ili kuviwezesha kutekeleza majukumu yake .Awamu ya pili itahusisha kupeleka pikipiki kwenye vyuo vingine 11” alisisitiza Kusaya. Saba , wizara ya kilimo ni kukarabati miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya kilimo ili majengo na vifaa vya kufundishia yawe ya kisasa na kusaidia kuboresha ufundishwaji. Mpaka sasa Kusaya alisema amekwishatembelea vyuo vya mafunzo ya kilimo 12 kati ya 14 tangu alipoteuliwa mwezi Machi mwaka huu ambapo amegundua kuwa kuna uhitaji mkubwa wa kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini. Katika hatua nyingine Kusaya alitembelea na kukagua utendaji kazi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Dakawa wilaya ya Mvomero na kukipongeza kituo hicho kwa kuongeza uzalishaji mbegu bora za mpunga . “ Nawapongeza TARI Dakawa kwa kuongeza uzalishaji mbegu bora za mpunga toka tani 75.6 mwaka 2015/16 hadi tani 93.7 mwaka 2019/20 hali iliyosaidia kukuza tija na uzalishaji mpunga nchini” alisema Kusaya Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt.Geofrey Makamilo alisema taasisi hiyo inaendelea kujikita kuhakikisha utafiti na upatikanaji mbegu bora za mazao unaimarika na kuwa tayari mwaka huu wamepokea Shilingi Bilioni 1.4 kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za michikichi ili kugawa kwa wakulima. Dkt.Mkamilo alibainisha pia TARI wamepokea Shilingi Bilioni 1.76 mwaka huu 2020 kwa ajili ya kuzalisha mbegu begu bora za zao la mkonge mkoani Tanga. “ Jumla ya hekta 30.2 za mbegu ya mkonge zimelimwa katika kituo cha utafiti Mlingano na miche milioni 2.4 imekwisha zalishwa na itagawiwa kwa wakulima katika mikoa 17 inayolima mkonge nchini” alisema Dkt.Mkamilo. Katibu Mkuu Kusaya alitembelea pia kituo cha utafiti wa kilimo TARI Ilonga wilayani Kilosa na kujionea kazi ya uzalishaji miche bora ya michikichi ipatayo 600,000 itakayogawiwa kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro ili kupanda. Alikipongeza kituo hicho na kutoa wito wa kuongeza kasi ya kuzalisha mbegu bora ya michikichi aina ya Tenera yenye kutoa mafuta mengi ili kutimiza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuifanya nchini iondokane na utegemezi wa mafuta ya kula toka nje ya nchi. “Tanzania kwa mwaka tunatumia shilingi bilioni 443 kuagiza mafuta ncje ya nchi wakati tunayo ardhi inayofaa kwa kilimo cha mazao ya mafuta kama michikichi, alizeti na karanga. TARI endeleeni kuzalisha miche mingi bora ya michikichi kwa ajili kugawa kwa wakulima” alisema Kusaya Kusaya alisema wizara ya Kilimo itaendelea kuhakikisha mahitaji ya kifedha na vifaa kama matrekta kwa taasisi ya utafiti wa kilimo ikiwemo upatikanaji wa maabara bora kwa kila kituo kwa ajili ya kupima afya ya udongo na kushauri wakulima zinapatikana.