Na. Hassan Mabuye, Mbeya
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amezindua mpango wa kitaifa wa kuwakopesha wananchi fedha za kufanya urasimishaji wa maeneo yao kwa kipindi cha miaka miwili.
Waziri Lukuvi ameyasema hayo katika kata ya Igawa wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya wakati akizindua Mpango wa maalumu wa kukopesha wananchi gharama ya kupanga, kupima na kupewa hati kwa kushirikiana na Benki ya NMB.
Lukuvi amesema mpango huu ni wa nchi nzima ambao umeanzia hapa Mbarali kwa kuwamilikisha wananchi zaidi ya 52,000 kwa kuwa mazoezi mengi ya urasimishaji yameshindwa kufanikiwa kwa sababu baadhi ya wananchi wameshindwa kupata fedha kwa mkupuo kugharimia shilingi 150,000 za upimaji na umilikishaji.
“nimeamua kuanzisha mpango huu kwa kushirikiana na NMB ambao watawakopesha fedha za kupanga, kupima na kuandaa hati ambazo Benki italipa 100% kwa mkupuo kisha nyinyi mtalipa taratibu na kwa awamu kwa muda wa miezi 24 yaani miaka miwili”, amesema Waziri Lukuvi.
“Baadhi ya wananchi wamekwamisha kazi hii ya urasimishaji katika maeneo mengi kwa kuwa wachache ndio wameweza kupata fedha za kugharamia upangaji, upimaji na umilikishaji kwa wakati. Sasa NMB leo hapa Mbarali wamekuja kuwakopesha wananchi gharama zote. na ninataka zoezi kama hili lifanyike nchi nzima na wengine waige kwa kuufuata utaratibu huu", ameongeza Waziri Lukuvi.
Amesema pia 90% ya wananchi wa Mbarali walikuwa hawakopesheki kwa sababu ya ardhi yao ilikuwa haijapangwa wala kupimwa. Lakini kwa mpango huu pia watakuwa na haki ya kukopeshwa na benki yoyote hapa nchini kwa kuwa watakuwa na dhamana inayotambulika kisheria ambayo ni hatimiliki ya ardhi.
Naye Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Bwana Benedicto Baragomwa amewataka wananchi kuchangamkia fursa hii kufanya urasimishaji kupitia Benki ya NMB ambayo itafanya zoezi hili kwa kutumia matawi yake yote 226 nchi nzima kujipatia mkopo huu na kujiwezesha kiuchumi.
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Mary Makondo amewahakikishia wananchi kwamba Wizara yake itasimamia kikamilifu mpango huu ambao wananchi watapewa hatimiliki za ardhi za miaka 99 na watamilikishwa kisheria.