Jonas Kamaleki, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia viongozi wa dini kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika shughuli za maendeleo nchini.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) unaofikia kilele chake leo.
”Dini zina mchango mkubwa kwenye ustawi na maendeleo ya nchi kutokana na namna zinavyoshirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi kimwili hasa katika masuala ya kijamii”, alisema Rais Magufuli.
Rais aliishukuru TAG kwa kuwahudumia wananchi kwa kujenga vyuo vitano vya ufundi, shule za sekondari tat zikiwemo nane ambazo zinakamilishwa kujengwa, shule za msingi nane, chekechea 117, vituo vya watoto yatima na wa mitaani 21, miradi ya kijamii 77 na kuchimba visima 201.
“Sio rahisi kuzungumzia maendeleo ya nchi yoyote ikiwemo Tanzania bila kugusia mchango wa taasisi za kidini, hii ni kwa sababu dini zinatoa mchango mkubwa kwa ajili ya huduma hasa za kiroho kwa kwa kuhimiza upendo, amani, umoja, kujenga maadili mema kwa wannanchi pamoja na kuwafanya raia wema wenye kuwajibika kwa jamii na taifa lao”, alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameliasa Kanisa la TAG pamoja na kujenga chuo kikuu, watenge eneo jingine kwa ajili ya kujenga viwanda ili kutengeneza ajira kwa wananchi na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ili kuziwezesha taasisi za dini kuendelea kuchangia maendeleo ya nchi hususan uwekezaji.
Akizungumzia baadhi ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali imekarabati na kuwezesha treni kufika Arusha baada ya kusimama kwa takribani miaka 30, inajenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji utakaozalisha megawati 2115 na imerudisha nidhamu ya watumishi Serikalini.
Ameongeza kuwa miradi yote hiyo imewezekana kwa kuwa watanzania na viongozi wa dini wamemtanguliza Mungu katika maslahi mazima ya Taifa.
“Tunamshukuru Mungu kwa kusikia kilio chetu na kutuondolea ugonjwa wa COVID-19, sasa Tanzania iko salama. Hili ni fundisho kwetu wanadamu kuwa tukipata mitihani mikubwa tusitegemee akili zetu pekee bali tumshirikishe Mungu kwa sababu kwake hakuna kinachoshindikana”, alisisitiza Rais Magufuli.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Rais aliwaomba watanzania wamwombe Mungu ili wapatikane viongozi wenye maono, wachakazi, wazalendo na wasio vibaraka.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dkt. Barnabas Mtokambali, alimpongeza Rais Magufuli kwa uchapakazi wake makini, shupavu na wa kuigwa ambao amesema umeleta maendeleo makubwa ndani ya nchi kwa kipindi kifupi.
“Nakupongeza wewe na Serikali yako kwa maono makubwa juu ya nchi yetu na watu wake ambayo yanaitikisa dunia, kupitia utawala wakoumewezesha kuongeza na kudumisha nidhamu kwa watumishi wa umma pamoja na kupambana na rushwa za aina mbalimbali”, alisema Askofu Dkt. Mtokambali.
Aidha, kutokana na utendaji wa Rais Magufuli na hasa alivyolishughulikia janga la Corona kwa kumtanguliza Mungu, Baraza Kuu la Kanisa la TAG limemtunuku tuzo maalum Rais Magufuli.
Askofu Dkt. Mtokambali amempongeza pia Rais Magufuli na Serikali yake kwa kubuni na kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo kwa hali ya kawaida kwa mujibu wa Askofu Mtokambali ingetekelezwa kwa muda wa miaka 40. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere, ujenzi wa hospitali na vituo vya fya na miradi ya maji mijini na vijijini.
Mkutano Mkuu wa Kanisa la TAG umefanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 9 hadi 14. Umejumuisha maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa idara mbalimbali za kanisa hilo.