Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yazibana Wizara na Idara Zake Kukusanya Mapato Yasiyo Kodi kwa Ufanisi
Jun 03, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Sera, Bw. Lawrence Mafuru, amezitaka Wizara na Idara zinazojitegemea zinazokusanya mapato ya Serikali yasiyo Kodi, kuhakikisha kuwa wanakusanya maduhuli hayo kwa ufanisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yatakayoisaidia kuwaletea wananchi maendeleo mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023.

Bw. Mafuru ametoa maelekezo hayo alipokutana na kujadiliana na wadau kutoka Wizara na Taasisi 25 za Serikali zinazotoa mchango katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa kukusanya maduhuli ya Serikali kila mwaka wa fedha.

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, makadirio ya mapato yasiyo kodi yalikuwa shilingi trilioni 2.92 sawa na asilimia 8.4 ya Bajeti yote ya Serikali ya shilingi trilioni 34.88 ambapo mapato halisi yalikuwa shilingi trilioni 2.21 sawa na asilimia 75.6 ya lengo lililokusudiwa.

Bw. Mafuru alisema kuwa mwaka ujao wa fedha 2022/2023, Serikali inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 3 za mapato yasiyo kodi na kuzitaka Wizara na Idara za Serikali kuimarisha mifumo ya ukusanyaji pamoja na kusimamia  ipasavyo mapato hayo.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, alizitaka Wizara na Idara hizo zinazotakiwa kuiwezesha Serikali kupata mapato ya kutosha ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi, kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, amezitaka, Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zilizopokea fedha za kukabiliana na athari za Uviko 19 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa- IMF, kuwasilisha katika Wizara ya Fedha na Mipango mikataba yote waliyoingia na wazabuni waliotekeleza miradi hiyo.

Alisema kuwa kuna kusuasua kwa uwasilishaji wa mikataba hiyo hatua ambayo inakiuka makubaliano ya kimkataba yaliyoingiwa kati ya Serikali na IMF, hatua iliyolenga kuweka uwazi wa matumizi ya fedha hizo na kuzitaka Wizara, Idara na Taasisi hizo kutekeleza maelekezo hayo haraka iwezekanavyo.

Hivi karibuni, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) liliipatia Tanzania mkopo usio na riba wenye thamani ya shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19 na miongoni mwa masharti ya mkopo huo ni kuwepo kwa uwazi wa matumizi ya fedha kwa umma na kuweka bayana mikataba iliyoingiwa na wazabuni pamoja na wakandarasi mbalimbali waliotekeleza miradi inayohusiana na mkopo huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi