Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaweka Wazi Mafanikio Ujenzi wa Miundombinu ya Kisasa ya Barabara
Feb 17, 2025
Serikali Yaweka Wazi Mafanikio Ujenzi wa Miundombinu ya Kisasa ya Barabara
Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Elphatar Mlavi akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Februari 17, 2025 jijini Dodoma.
Na Mwandishi wetu- Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuimarisha miundombinu nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025 kwa kujenga miundombinu ya kisasa ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Elphatar Mlavi wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Februari 17, 2025 jijini Dodoma.

“Barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami,” amesema Mlavi

Ameongeza kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja 10 unaendelea akiongeza kuwa miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba (7) ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina  ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami.

“Katika kipindi cha miaka minne (Juni 2021 – Des. 2024) hali ya barabara kuu na zile za mikoa imeendelea kuimarika ambapo barabara zilizo katika hali nzuri na wastani zimekuwa karibu asilimia 90 ya jumla ya mtandao wote wa barabara wenye Kilometa 37,225.72”, amesema Mhandisi Mlavi.

Amesema katika kipindi tajwa madaraja makubwa 9 yamekamilika kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 381.301  katika eneo la Gerezani (Dsm), Daraja jipya la Tanzanite  (Dsm), Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida).

Aidha, madaraja mengine 10 ambayo ni Kigongo – Busisi (Magufuli Bridge - Kilometa 3.0), Lower Mpiji (Meta 140), Mbambe (Meta 81), Simiyu (Meta 150), Pangani (Meta 525), Sukuma (Meta 70), Kerema Maziwani (meta 80), Kibakwe (meta 30), Mirumba (Meta 60) na Jangwani (Meta 390) ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 985.802.

Kuhusu madaraja makubwa kumi na tisa (19) ambayo yako kwenye maandalizi ya kujengwa, Mhandisi Mlavi ameyataja kuwa ni Godegode (Dodoma), Ugala (Katavi), Kamshango (Kagera), Bujonde (Mbeya), Bulome (Mbeya), Chakwale (Morogoro), Nguyami (Morogoro), Mkundi (Morogoro), Lower Malagarasi (Kigoma), Mtera (Dodoma), Kyabakoba (Kagera), Mjonga (Morogoro), Doma (Morogoro), Sanga (Songwe), Kalebe (Kagera), Ipyana (Mbeya), Mkondoa (Morogoro), Kilambo (Mtwara) na Chemchem (Singida).


Kwa upande wa ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa nje (Outer Ring Road)  katika jiji la Dodoma kwa kiwango cha lami yenye jumla ya urefu wa Kilometa 112, inayolenga kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji, hadi kufikia Februari, 2025, ujenzi umefikia asilimia 91 sehemu ya kwanza (1) ya Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Bandari Kavu (km 52.3) na (km 85) kwa Sehemu ya Pili (2) ya Ihumwa Bandari Kavu – Matumbulu – Nala (km 62).

Katika kupunguza foleni ya magari katika mizani zenye magari mengi, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS imefunga mizani ishirini (20) za kupima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh-in-Motion WIM) katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Songwe, Dodoma, Singida, Arusha na Mara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi