Serikali imewahakikishia wadau wa usafiri na usafirishaji wanaotumia bandari ya Dar es Salaam kuwa iko tayari wakati wote kuhakikisha inaboresha mifumo na miundombinu ya bandari ili kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi na hivyo kuvutia watumiaji wengi zaidi.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wadau hao jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire, amesema Serikali inafuatilia kwa karibu changamoto zote zinazojitokeza katika usafirishaji ili kuhakikisha wanufaika ambao ni wafanyabisha wa ndani na nje ya Tanzania hawapati kikwazo na kuacha kutumia bandari ya Dar es Salaam.
“Niwahakikishie kuwa Serikali inafuatilia kwa karibu changamoto zote zinazojitokeza katika matumizi ya bandari na hiyo inafanyika kwa kufanya vikao na kuchukua hatua kwa kila changamoto inayojitokeza", amesema Katibu Mkuu huyo.
Katibu Mkuu huyo ameipongeza Serikali ya Zambia kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania hasa pale ilipotokea changamoto ya mgomo wa madereva katika mpaka wa Nakonde nchini Zambia na kusababisha bidhaa kucheleweshwa kwa walaji.
Aidha, Migire amechukua nafasi hiyo kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kubuni mifumo itakayowawezesha madereva wanaochukua mizigo bandarini kufuatilia mizigo wanayochukua bila kupata changamoto yoyote ili kuwapunguzia muda wa kukaa ndani ya bandari.
“TPA lazima muwe wabunifu mkajifunze kwa wenzenu bandari nyingine, kwa bandari yetu hii mkiweka mifumo hasa kwenye kuchukua mizigo mtapunguza sana magari kukaa bandarini na mifumo hiyo itawarahisishia madereva wanapoingia wajue mizigo wanaichukua wapi na kisha kuipelekea inapotakiwa kwenda”, amesisitiza Migire.
Kwa upande wake Mwenyekti wa Chama cha Madereva Tanzania (ITDA), Adam Mwenda, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuchukua hatua stahiki na kwa wakati dhidi ya mgomo wa madereva uliotokea katika Mpaka wa Tanzania na Zambia.
Mwenyekiti Mwenda ameiomba Serikali kufuatilia kwa karibu changamoto mbalimbali ambazo Serikali mbili zimekubaliana katika kikao chao ili kufanya biashara baina ya Tanzania na nchi jirani iweze kufanikiwa zaidi kwani wateja wakubwa wa bandari ya Dar es salaam ni Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Serikali kupitia Sekta ya Uchukuzi imekuwa na mpango kazi wa kufanya vikao vinavyowahusisha wadau wote wa bandari ya Dar es Salaam kila mwezi ili kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi na kukuza uchumi wa nchi.