Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkataba wa Ujenzi Bomba la Mafuta Hoima-Tanga Watua Bungeni
Sep 12, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Serikali imewasilisha Mkataba wa Kimataifa wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Akiwasilisha Mkataba huo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Tanzania na Uganda ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo malengo yake ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama kwenye maeneo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii kiteknolojia , utafiti, ulinzi na masuala ya Kisheria.
Dkt. mwakyembe amesema kuwa Serikali ya Uganda kupitia kampuni za Kimataifa za TOTAL, TULLOW NA CNOOC iligundua uwepo wa mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5 katika eneo la Albertine nchini Uganda.
" Kufuatia ugunduzi huo, Serikali ya Uganda ilianza kutafuta njia ya kusafirisha mafuta hayo kwenda kwenye soko la kimataifa ambapo iliaanisha njia takribani tatu ikiwemo ile ya kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania" amesema Dkt. mwakyembe.
Aidha Dkt. mwakyembe amebainisha baadhi ya faida zitokanazo na Mkataba huo ikiwemo kuongezeka kwa mapato ya Serikali kutokana na Kodi ya zuio na Kodi ya Mapato ya Kampuni zitakazotozwa wakati wa ujenzi na uendeshaji wa Mradi.
Vilevile amesema kuwa Serikali ya Tanzania itanufaika katika kuongezeka kwa mapato ya Serikali kwa takribani Dola za Marekani 12.2 kwa kila pipa la mafuta ghafi litakalosafirishwa kupitia Bandari ya Tanga kulingana na kiwango cha Hisa za Serikali ya Tanzania.
" kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia, ulinzi na usalama kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla sambamba na kuimarika kwa huduma mbalimbali katika bandari ya Tanga kutokana na shughuli za Mradi na miundombinu itakayojengwa" aliongeza Dkt. Mwakyembe
Pia ongezo kwa fursa za  ajira kwa Watanzania ambapo takribani watanzania 10, 000 wataajiriwa wakati wa ujenzi na ajira zipatazo 1,000 wakati wa uendeshaji, Amesema Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake Deogratius Ngalawa akimuwakilisha  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ameishauri Serikali kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa mkataba huo kwa kuzingatia mustakabali wa manufaa ya kiuchumi kwa Taifa.
" Napenda kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake na umahiri aliouonesha katika kuhakikisha Tanzania inapata fursa ya mradi huu mkubwa wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania" Amesema Ngalawa.
Akiongea kwa niaba ya Msemaji Mkuu kambi Rasmi ya Upinzani Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Devota Minja amesema kuwa bomba hilo la kusafirisha mafuta ilikuwa na kazi iliyohusu zaidi ushawishi mpana kwani kulikuwa na ushindani mkubwa utoka kwa nchi jirani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi