Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yawalipa Wazabuni Tril 2.1 kwa Mwaka 2016 Hadi 2023
Jan 30, 2024
Serikali Yawalipa Wazabuni Tril 2.1 kwa Mwaka 2016 Hadi 2023
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, kuhusu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki, bungeni Jijini Dodoma.
Na Khadija Ibrahim, WF, Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu ameliambia Bunge, mjini Dodoma kuwa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi Desemba 2023, imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani zaidi ya shilingi trilioni 2.1 kati ya madai ya zaidi ya shilingi trilioni 3.1 yaliyowasilishwa.

 

Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, aliyetaka kufahamu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa ama kukataa kuwalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki.

 

“Jumla ya madeni ya  wazabuni na wakandarasi yaliyowasilishwa kwa uhakiki yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 3,110.33kati ya kiasi hicho madeni yaliyolipwa ni zaidi ya shilingi bilioni 2,128.54 ambapo shilingi bilioni 1,032.13 ni madeni ya wazabuni na shilingi bilioni 1,096.41 ni madeni ya wakandarasi”, alisema Dkt. Nchemba

 

Alisema kuwa madeni ya shilingi bilioni 981.79 yalikataliwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa nyaraka, madeni kubainika kulipwa tayari, pamoja na makosa ya ukokotoaji. 

 

Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo na uchumi wa Taifa, imeendelea kutenga na kulipa madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyohakikiwa na kukubaliwa.

 

Alifafanua kuwa Serikali, imeongeza bajeti ya kulipa madeni kutoka wastani wa shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 700 kwa mwaka na kuahidi kuwa  madai ya wazabuni na wakandarasi yataendelea kulipwa kadri watakavyowasilisha hati zao za kukamilisha kazi (certificates).

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi